March 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WMA:Wananchi nunueni kokoto,mchanga kwa kuzingatia mita za ujazo

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

AFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipomo (WMA),Alban Kihulla amewaasa wananchi  kununua kokoto,kifusi na mchanga kwa kuzingatia mita za ujazo na siyo kwa tripu kama wengi walivyozoea.

Kihulla ametoa ushauri huo leo jijini hapa Machi,25,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya serikali ya awamu ya sita,ambapo amesema ununuaji huo kokoto,kifusi na mchanga kwa kutumia tripu siyo sahihi hivyo ni vyema mtu anayeagiza bidhaa hiyo akapanga bei na muuzaji kwa kuangalia mita za ujazo kwenye tipa la gari linalobeba ili kupata bei halisi.

Kihulla amesema WMA imeendelea kuwalinda wanunuzi kwa kuhakikisha bidhaa wanazonunua zinakuwa kwenye kipimo sahihi hivyo ni vyema kila mwananchi akajiridhisha na bidhaa anayotaka kabla ya kuinunua na akihisi haipo katika kipimo sahihi atoe taarifa kwa wakala hiyo ilikujiridhisha.

“Wakala imeendelea kununua vifaa vya kitaalam kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo Iron Weight 500kg (100) kwa ajili ya kufanyia uhakiki na ukaguzi wa mizani kubwa zinazotumika viwandani na kwenye barabara na mitambo mikubwa miwili na mitambo midogo 10 inayobebeka kwa ajili uhakiki dira za maji,”amesema Kihulla.

Aidha Kihulla amesema Wakala hiyo imenunua mitambo 12 kwa ajili ya kuhakiki vipima mwendo kwenye vyombo vya usafiri, kati ya mitambo hiyo, mitambo 10  inabebeka ambayo itasambazwa kwenye mikoa.

Vile vile,imenunua mitambo miwili ya kusimika ambapo mtambo mmoja unaendelea kusimikwa katika kituo cha uhakiki wa Vipimo Misugusugu na mtambo mwingine utasimikwa katika ofisi ya Makao Makuu Dodoma.

“Wakala imenunua mita nne za mtiririko kwa ajili ya kuhakiki mita zilizofungwa kwenye maghala ya kuhifadhia mafuta, migodini, viwanja vya ndege na sehemu nyingine zinazotumika kujaza mafuta kwa kasi kubwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa mita hizo zinatoa vipimo sahihi vya kiasi cha mafuta,”amesema.

Pamoja na hayo Kihulla amesema kuwa kuanzia mwaka 2021/22 hadi Februari, 2025, Wakala imechangia jumla ya shilingi bilioni 17.1.

Aidha amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25, Wakala inatarajia kuchangia kwenye mfuko Mkuu wa Serikali zaidi ya shilingi bilioni 7 ambapo kufikia Februari, 2025, Wakala imechangia kiasi cha shilingi bilioni 3.8.

Hata hivyo Kihulla amesema Wakala hiyo imefanikiwa kuhakiki vipimo 3,668,149 vitumikavyo katika sekta mbalimbali nchini kati ya vipimo 3,923,652 ilivyopanga kuhakiki ambayo ni sawa na asilimia 94 ya lengo.

“Kati ya vipimo hivyo vilivyohakikiwa, vipimo 102,969 vilikutwa na mapungufu ambayo yalirekebishwa na kuruhusiwa kuendelea kutumika na vipimo 5,607 vilikataliwa kutumika baada ya kuonekana na mapungufu ambayo hayarekebishiki,”amesema Kihull.

Pia ameeleza kuwa Wakala hiyo imejenga majengo mapya ya ofisi katika Mkoa wa Mara na Simiyu. Vile vile, ujenzi wa ofisi hizo umefanyika katika Mkoa wa Dodoma ambapo ujenzi wa jengo ambalo sasa linatumika kama ofisi za Wakala wa Vipimo Makao Makuu ulikamilika Machi, 2025 kwa shilingi billion 6.99.