December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Pwani, Alban Kihula (Kulia) alimfafanulia Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe (Katikati) namna wanavyopima mita za maji kabla ya kwenda kwa watumiaji wa mwisho. Anayefuata ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa WMA Dk. Ludovick Madege na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ludovick Nduhiye.

WMA kuanza kupima mita za umeme Oktoba

Na Mwandishi Wetu

WAKALA wa Vipimo nchini (WMA), unatarajia kuanza kupima mita za umeme kuanzia Oktoba mwaka huu ili kuwawawezesha watumiaji wa nishati hiyo kuwa na uhakika wa kiasi wanachotumia na wanacholipia.

Hayo yamesemwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Dk. Ludovick Manege, wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe.

Profesa Shemdoe ametembelea kituo cha kupima kiasi cha mafuta kwenye matenki ya malori na mita za maji cha WMA kilichoko Misugusugu Mkoa wa Pwani kuangalia utendaji kazi wa kituo hicho.

Dkt. Manege amesema mkandarasi wa kuleta mtambo huo ambaye ni mjerumani amemhakikishia kuwa mtambo huo utakuwa umefika na kusimikwa Oktoba mwaka huu.

Amesema mtambo huo utagharimu sh. milioni 600 na kwamba kwa sasa WMA inashughulikia jengo ambalo mtambo huo utawekwa utakapowasili ili uweze kuanza kazi haraka.

“Tunataka uchaguzi ukimalizika tu basi mtambo uwe umeshaanza kufanyakazi kwasababu tunataka kuhakikisha mtumiaji wa mita hizo anapata kiwango sahihi cha umeme na analipa kiwango sahihi bila kupunjwa,” amesema

Aidha, amesema mbali na kupima mita za maji na umeme wako mbioni kuanza kupima ujazo sahihi wa gesi lengo likiwa lile lile kuhakikisha wananchi wanapata ujazo unaostahili.

“Tumeona bajeti kubwa ya utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa maji na mradi wa umeme wa Rufiji na nchi inajielekeza kwenye utekelezaji wa miradi ya gesi sasa sisi WMA lazima tujipange kuhakikisha wananchi wanapata maji, umeme na gesi kwa vipimo sahihi na kupila viwango sahihi,” amesema

Kwa upande wake, Profesa Shemdoe amesema amejionea namna mita za maji zinavyopimwa kuwahakikishia vipimo sahihi wananchi na malori ya mafuta ili kupata vipimo sahihi.

Alisema kazi hizo hazifanyiki bure kwani kwa kila mita serikali imekuwa ikipata 10,000 hivyo kila mita inayoingia nchini inapaswa kupitia WMA kwaajili ya kukaguliwa kama iko sawa.

“Hawa wameanza ununuzi wa mtambo wa kupima mita za umeme sasa naomba mchakato huo ufanyike haraka mtambo uje ili wenzetu wa Tanesco nao walete mita zao zihakikiwe hapa,” alisema Shemdoe

Ameagiza pia WMA ianze mchakato wa kuagiza mtambo kwaajili ya kupima mita za gesi zinazotumika kwenye viwanda na maeneo mengine ili wananchi walipe kile wanachotumia.

“WMA mhakikishe mnashirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kuhakikisha mchakato wa kuleta mtambo wa gesi unafanyika ili kuhakikisha wananchi wanalipa kile wanachotumia,” alisema Prof. Shemdoe.