Na Grace Gurisha, TimesMajira Online
MRATIBU wa Miradi inahusiana na ulinzi wa Wanawake na Watoto katika Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC), Consolatha Chikoti amesema kunatakiwa kuwepo na jitihada mbalimbali za Serikali na wadau wa mendeleo ya kijamii kutokomeza ukatili hasa kwa watoto ambao wanatajwa kwenye kundi lililopo katika hatari ya kufanyiwa ukatili.
Chikoti amesema hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa WLAC, Theodosia Muhulo wakati wa kuadhimisha siku ya mtoto wa kike iliyofanyika katika Shule ya Msingi Annex, iliyopo Manispaa ya Temeke, Mbagala jijini Dar es Salaam.
Amesema, watoto wana haki ya kulindwa ili watimize ndoto zao kwani kuna baadhi ya watoto wa kike waliyofanyiwa ukatili wa kijinsia ambao wameshindwa kuendelea na shule kutokana na mazingira yaliyowazunguka.
Chikoti ambae pia ni Mratibu wa Tamasha hilo amesema, mradi huo unatekelezwa katika Wilaya za Ubungo, Temeke na Kinondoni ambapo ni mradi kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa watoto.
“Watoto ni kundi ambalo lipo kwenye hatari ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia hivyo kunatakiwa kuwepo na jitiada za haraka kutoka Serikali na kwa wadau wa maendeleo ya jamii pamoja na asasi za kitaifa kuhakikisha zinahusika moja kwa moja katika ulinzi wa mtoto,” amesema Chikoti.
Afisa Elimu Msaidizi Kata ya Mbagala, Mwalimu Jemima Lenjima amesema, ukatili kwa watoto upo na hali siyo nzuri sababu watoto wanatoka mitaani hivyo wazazi na jamii kwa ujumla wanatakiwa kushirikiana kutoa taarifa za ukatili huo.
“Mtoto anapokueleza kwamba amepata tatizo, jaribuni kulifuatilia kuanzia ngazi ya chini na kama alipata tatizo akiwa shuleni basi waliripoti kwa walimu lakini kama ni nyumbani basi kuna ngazi mbalimbali za kuanzia ikiwemo Serikali za Mitaa hadi kufika Polisi,” amesema Lenjima.
Lakini pia amesema, tangu watoto hao wapewe mafunzo kwa kushirikiana na WLAC
kumekuwa na mabadiliko makubwa kwa sababu watoto wameweza kujitambua, wamepunguza uoga na kupata ujasiri wa kueleza tatizo pindi tu linapompata bila ya kuona aibu.
Kwa upande wake Getrude Nyagabona ambaye ni Ofisa Ustawi wa Jamii, Kata ya Mbagala amesema, wao ndiyo wanaohusika katika masuala ya ulinzi na usalama wa mtoto na katika maadhimisho ya mwaka huu yenye kauli mbio isemayo ‘Sauti yangu kwa kesho yenye sawa’ ikiwa na maana ya tumsikilize mtoto wa kike kwa sababu yupo kwenye kundi ambalo ni hatarishi.
Mmoja wa wazazi waliohudhuria maadhimisho hayo, Tekla Elieza amesema, mtoto wa kike anakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo mara nyingi zinasababisha watoto hao kuingia kwenye mazingira hatarishi na vishawishi.
“Mfano kwa binti anasoma shule iliyo umbali mrefu huwa anakutana na vijana wa bodaboda ambao huwadanganya kwa kushawishi kumpeleka shuleni ama kurudisha nyumbani, na kwa kuwa mtoto anakuwa ameishatembea sana, anakubali kupanda bodaboda na kujikuta
amepelekwa mahali pengine na kufanyiwa vitendo vya ukatili,” amesema na kuongeza.
“Msaada unaotolewa na WLAC umetusaidia sana sisi kama wazazi na umetufanyia wepesi wa kuweza kufuatilia watoto wetu na tukienda kwenye vyombo husika tunasikilizwa, nina washauri wazazi ambao bado hawajajiongeza, wajiongeze ili tuweze kuwalinda watoto wetu wa kike,”amesema mzazi huyo.
Afisa Elimu Kata ya Mbagala, Jemima Lenjima akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kuadhimisha siku ya mtoto wa kike na jinsi walivyojipanga kuwasaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao.
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Leah Mbunda kutoka Dawati la Jinsi na Watoto Kanda maalumu Dar es Salaam, amesema katika kuhakikisha ulinzi wa watoto unakuwepo, dawati linahakikisha linashughulikia makosa yanayohusiana na ukatili huo kwa haraka.
“Dar es Salaam tuna madawati zaidi ya 20 na wahudumu ni askari waliopata mafunzo waliotapakaa katika vituo vya polisi vikubwa ili kuwashughulikia wahanga wa ukatili. Tunashukuru sana WLAC kwa kutoa elimu imesaidia sana, wananchi wamepata mwamko, wamepata uelewa wa kutumia madawati yetu,” amesema Mrakibu Mbunda
Ameongeza kuwa, pamoja na kupokea malalamiko mengi pia wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali, ambapo kesi nyingi zinazoripotiwa hazifiki mwisho mzuri, kwa sababu zikishafika mahakamani wahanga hawaonekani.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â