Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Dodoma
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Mariam Ditopile, ameipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuendana na kasi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha uwekezaji katika sekta za viwanda na biashara unakuwa na tija, kuchochea ajira mpya, na kuinua hali ya uchumi kwa kila Mtanzania.
. Ditopile alitoa pongezi hizo jijini Dodoma wakati wa mafunzo kwa Kamati hiyo yaliyotolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara, ambapo alieleza kuwa mafanikio ya sekta hizo ni kichocheo kikuu cha uchumi wa Taifa.
“Tunapongeza jitihada za Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha uwekezaji unaongezeka na kuleta matokeo chanya kwa jamii,” alisema Mhe. Ditopile.
Aidha, Kamati hiyo ilitoa maoni, maelekezo na mapendekezo kwa Wizara, ikisisitiza umuhimu wa Wizara kushuka zaidi katika maeneo ya uzalishaji na kuwa karibu na wafanyabiashara pamoja na wamiliki wa viwanda ili kufahamu kwa undani changamoto na fursa zilizopo.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo, alieleza kuwa dhamira kuu ya Wizara ni kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi muhimu barani Afrika katika mageuzi ya maendeleo kupitia viwanda na biashara.
Katika kikao hicho, Kamati pia iligusia changamoto ya ongezeko la matumizi ya pombe kupita kiasi, na kuipongeza Wizara kwa kushirikiana na taasisi kama TBS na Wakala wa Vipimo kufanya tafiti na kuweka mifumo ya udhibiti. Hata hivyo, Kamati ilisisitiza umuhimu wa mabadiliko ya tabia kwa wananchi, hususan vijana, kuhusu matumizi sahihi ya pombe.
“Ni jukumu la kila Mtanzania kuwaelekeza vijana kunywa pombe kwa kiasi. Lengo ni kulinda afya zao, maendeleo ya jamii, na mazingira bora ya uwekezaji nchini,” ilisisitiza Kamati hiyo.
Kamati hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na Wizara hiyo kuhakikisha sera na mikakati inayoandaliwa inaleta matokeo chanya na ya kudumu kwa wananchi.
More Stories
EWURA yaombwa kuongeza elimu kuhusu nishati safi ya kupikia
Wataslam Mifumo ya NeST wanolewa
Ngozi:Wanawake nchini wanakila sababu ya kumshukuru Rais Samia kutoa nafasi za uongozi kwao