March 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya nishati yapokea Tril.1.15 za miradi ya Maendeleo

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

WIZARA ya Nishati imepokea Sh. trilioni 1.150 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, sawa na asilimia 61 ya bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Taarifa hiyo imetolewa Machi 10, 2026 na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya sekta ya nishati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini inayoongozwa na Mwenyekiti wake,Subira Mgalu, katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Ndejembi amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 wizara imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini.

Amesema katika fedha zilizopokelewa hadi sasa, Sh. bilioni 410.04 ni fedha za ndani na Sh. bilioni 740.30 ni fedha za nje ambazo zimeendelea kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta ya nishati.

Ameongeza kuwa miradi hiyo inajumuisha upelekaji wa umeme vijijini na vitongojini, utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa za mafuta ya petroli pamoja na kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kwa mujibu wa Ndejembi, katika mwaka wa fedha 2025/26 Wizara ya Nishati iliidhinishiwa kutumia jumla ya Sh trilioni 1.965, ambapo Sh trilioni 1.886 sawa na asilimia 95.97 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo huku Sh bilioni 79.23 sawa na asilimia 4.03 zikiwa kwa matumizi ya kawaida.

Amefafanua kuwa kati ya fedha za maendeleo zilizoidhinishwa, Sh trilioni 1.466 ni fedha za ndani na Sh bilioni 420.49 ni fedha za nje.

Ndejembi ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa miongozo na maelekezo ambayo imekuwa ikitoa na kuchangia mafanikio katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesisitiza kuwa wizara itaendelea kupokea ushauri na maoni ya kamati hiyo pamoja na kutoa ushirikiano unaostahili ili kuimarisha maendeleo ya sekta ya nishati nchini.