November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Nishati yaahidi ushirikiano kwa watengenezaji wa magari ya umeme

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Arusha

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, amesema kuwa, Wizara ya Nishati itatoa ushirikiano kwa wabunifu pamoja na kampuni zinazotengeza magari yanayotumia umeme ili kuwezesha wananchi kuwa na vyanzo mbalimbali vya kuendesha magari badala ya kutegemea mafuta kama chanzo kikuu.

Alisema hayo tarehe 06 Juni, 2022 mkoani Arusha, wakati alipofanya ziara katika Shule ya Sayansi Arusha pamoja na kampuni ya kitanzania inayotengeneza magari ya umeme ya Hanspaul Group ili kuona ubunifu na pia kufahamu kama kuna changamoto zozote zinazohitaji utatuzi kutoka serikalini.

Akiwa katika Shule ya Sayansi Arusha, alielezwa na Mkuu wa Shule hiyo, Mary Mbise, kuwa, shule hiyo inafundisha Sayansi na Teknolojia kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita, ambapo wanafunzi hao wanapata nafasi ya kufanya ubunifu ili kuweza kusaidia jamii mara baada ya kuhitimu.

 Akiwa katika shule hiyo, Naibu Katibu Mkuu, alishuhudia ubunifu wa gari linalotembea kwa kutumia nishati ya umeme jua, printer ya 3D pamoja na jokofu linalotumia nishati hiyo ambalo lengo lake ni kuwasaidia wajasiriliamali wadogo wadogo hasa wanaouza mboga za majani ambapo badala ya mboga hizo kuzinyunyizia maji ili zisinyauke, zinawekwa kwenye jokofu hilo linaloitwa solar cooler house.

Naibu Katibu Mkuu aliwapongeza wanafunzi pamoja uongozi wa Shule hiyo kwa ubunifu wao na kueleza kuwa Wizara ya Nishati itawapa ushirikiano ikiwamo kuangalia fursa za kuongeza ujuzi kupitia miradi mbalimbali na uwekezaji.

Akiwa katika kampuni ya Hanspaul, Naibu Katibu Mkuu alishuhudia jinsi magari yanayotumia umeme yanavyotengenezwa ambapo alielezwa na Mkurugenzi Mkuu  wa kampuni hiyo, Satbir Hanspaul kuwa, magari hayo kwa sasa yameanza kutumika katika shughuli za utalii ambapo yanapeleka watalii katika mbuga mbalimbali ikiwemo Serengeti.

Hanspaul alisema magari hayo yameanza kutumika katika Sekta ya Utalii ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye amezidi kufungua fursa katika Sekta ya Utalii wa Tanzania kupitia Filamu ya Royal Tour.

Aliongeza kuwa, kampuni hiyo imeona fursa na kutengeneza magari yanayotumia umeme kwenda kwenye Mbuga za Wanyama ambapo magari hayo hayana uchafuzi wa mazingira, hayatoi kelele yanapokuwa mbugani na pia gharama zake za uendeshaji ni nafuu.

Hanspaul, alimshukuru Naibu Katibu Mkuu kwa kufanya ziara katika kampuni hiyo kwani  baada ya kuzungumza na watendaji wa kampuni hiyo ametoa muongozo ili teknolojia inayofanyika kiwandani hapo iwasaidie watanzania wengi zaidi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha Mjini,  Mhe.Mrisho Gambo alimpongeza Naibu Katibu Mkuu na ujumbe wake kwa kutembelea kiwanda hicho ili kufahamu masuala mbalimbali ikiwemo changamoto wanazopata na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi na kueleza kuwa, suala hilo linawafanya wadau mbalimbali wajenge imani zaidi kwa Serikali ya Awamu ya Sita.

Baada ya ziara kiwandani hapo, Naibu Katibu Mkuu aliwapongeza watendaji wa kampuni hiyo kwa teknolojia hiyo inayofanyika nchini Tanzania ambayo imetoa ajira kwa vijana wa kitanzania na kwamba changamoto mbalimbali zilizoelezwa na kampuni hiyo zitafanyiwa kazi na Serikali.

Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu aliambatana na Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Mrisho Gambo, Mkurugenzi wa Umeme kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Eng. Godfrey Chibulunje, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Arusha, Eng.Herini Mhina, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Eng.Barozi Patrick na Wataalam wengine kutoka EWURA na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (kushoto) akipata maelezo kuhusu mfumo wa gari linalotumia nishati ya umeme Jua ambalo limebuniwa na Wanafunzi katika Shule ya Sayansi Arusha iliyopo mkoani Arusha.
Gari linalotembea kwa kutumia nishati ya umeme Jua ambalo limebuniwa na Wanafunzi katika Shule ya Sayansi Arusha iliyopo mkoani Arusha.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali akiendesha gari linalotumia nishati ya umeme Jua ambalo limebuniwa na Wanafunzi katika Shule ya Sayansi Arusha iliyopo mkoani Arusha.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (wa Sita kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi kutoka Shule ya Sayansi Arusha waliobuni  gari linalotumia nishati ya umeme Jua. Wengine katika picha ni Watendaji wa Taasisi mbalimbali za Serikali ambao Naibu Katibu Mkuu aliambatana nao katika ziara yake.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (kulia) akizungumza na wanafunzi kutoka Shule ya Sayansi Arusha waliobuni jokofu linalotumia nishati ya umeme Jua ambalo linaweza kutumiwa na wajasiriamali wadogowadogo kuhifadhi mboga za majani zisiharibike.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (wa Saba kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi kutoka Shule ya Sayansi Arusha waliobuni jokofu linalotumia nishati ya umeme Jua ambalo linaweza kutumiwa na wajasiriamali wadogowadogo kuhifadhi mboga za majani zisiharibike. Wengine katika picha ni Watendaji wa Taasisi mbalimbali za Serikali ambao Naibu Katibu Mkuu aliambatana nao katika ziara yake.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (wa Pili kulia) akizungumza jambo wakati alipofanya ziara katika kampuni ya kitanzania inayotengeneza magari ya umeme ya Hanspaul Group. Kulia kwake ni Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Mrisho Gambo na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu  wa kampuni hiyo, Satbir Hanspaul.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (wa kwanza kulia) akitazama mfumo wa gari linalotumia umeme badala ya mafuta katika kampuni ya kitanzania inayotengeneza magari ya umeme ya Hanspaul Group iliyopo jijini Arusha. Wengine katika picha ni Watendaji kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali alioambatana nao pamoja na watendaji kutoka Hanspaul Group
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (kushoto) na Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe.Mrisho Gambo wakiwa katika moja ya magari yanayotumia umeme badala ya mafuta yanayotengenezwa katika kampuni ya kitanzania ya Hanspaul Group iliyopo jijini Arusha
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (Wa Tatu kutoka kulia), Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe.Mrisho Gambo (wa kwanza kushoto) wakionyesha moja ya magari yanayotumia umeme badala ya mafuta yanayotengenezwa katika kampuni ya kitanzania ya Hanspaul Group iliyopo jijini Arusha. Wengine katika picha ni Watendaji kutoka Hanspaul Group na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Umeme kutoka EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje.
Moja ya magari yanayotumia umeme yaliyotengenezwa na kampuni ya kitanzania ya Hanspaul Group ya jijini Arusha.