January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya michezo kumwaga neema kwa vyama, mashirikisho

John Mapepele, Arusha

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amesema, kuanzia mwaka huu Serikali itaanza kusaidia Mashirikisho na Vyama vya Michezo hapa nchini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ili Tanzania iweze kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa.

Gekul ameyasema hayo wakati akifunga mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza ya Netiboli yaliyomalizika jana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha ambapo amesisitiza kuwa kupitia bajeti ya mwaka huu wa fedha (2021-2022) Wizara imejipanga vyema kupitia mfuko huo kuzisimamia timu za Taifa na kuziwezesha kushiriki mashindano mbalimbali ya Kimataifa.

Katika mashindano hayo timu ya JKT Mbweni walifanikiwa kutetea ubingwa wao baada ya kuwafunga TAMISEMI Queens goli 40-39 wakati timu ya Smart kutoka Dar es Salaam ikiibuka washindi kwa upande wa wanaume.

“Natambua kuwepo kwa changamoto mbalimbali juu ya mchezo huu wa Netiboli ikiwemo kukosa Mlezi pamoja na Wafadhili. Hata hivyo tunawapongeza viongozi wa Chama kwa kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa,” amesema Naibu Waziri

Amesema, Wizara kupitia Idara ya Maendeleo ya Michezo ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Michezo, mpango ambao utasaidia kusukuma mbele maendeleo ya michezo hapa nchini ikiwemo mchezo wa Netiboli.

Amewataka viongozi wa vyama vya Michezo na Mashirikisho yote nchini kujipanga vyema katika kutekeleza Mpango huo.

Amesema kuwa, mwaka huu Wizara yake inaandaa Tamasha la Wanawake litakalokuwa kubwa na la aina yake ili kuleta hamasa kwenye michezo ya wanawake.

Amemshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kunipa jukumu la kushirikiana na viongozi wenzake katika kuisimamia michezo hususan michezo ya wanawake.

Amewapongeza viongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania na vilabu vyote vilivyoshiriki katika mashindano haya.

“Nazipongeza timu zote zilizoshiriki na wale wote waliofanikiwa kuibuka na ushindi kwa pande zote mbli za Wanawake na Wanaume”. Amefafanua Gekul

Amesema kupitia mashindano hayo ana imani watapatikana wachezaji wazuri, chipukizi na mahiri watakao saidia kuunda Timu ya Taifa itakayoshiriki mashindano mbalimbali na kuliwakilisha Taifa letu Kimataifa.

Pia ameupongeza Uongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kwa kuweza kuifuata kalenda yao ya mwaka na kuendesha mashindano, kozi na majukumu yao yote na kuwaomba wadau wengine wa Michezo kujitokeza kudhamini Mashindano haya ili kuendelea kuibua vipaji vya vijana.

Lakini pia ametoa mwezi mmoja kwa Mikoa yote kukamilisha uchaguzi wa viongozi wa CHANETA na baada ya hapo uchaguzi mkuu wa kitaifa ufanyike mara moja kwa kuwa hadi sasa ni mikoa minne tu ndiyo imekamilisha zoezi hili.

Aidha Gekul ametoa wito kwa wana michezo wote kuzingatia njia mbalimbali za kujikinga na Ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo amezitaka Wilaya zote nchini kuanzisha klabu za riadha kwa kuwa michezo inajenga afya, pia ametoa wito kwa Makatibu Tawala wa mikoa yote nchini kusimamia michezo na miundombinu ya michezo katika mikoa yao

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Sophia Mjema amemshukuru Gekul na kuiomba Serikali ifikilie kuturejesha mashindano haya mwakani mkoani Arusha ili kuendelea kuleta hamasa kwa wananchi wa mikoa ya kaskazini mwa Tanzania.