Na Jackline Martin,TimesmajiraOnline, Dar
WIZARA ya Maji imetekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuungana na nchi nyingine kuhakikisha suala ya ulindaji na utunzaji wa vyanzo vya maji linakua kipaumbele, ambapo Tanzania imetia saini mkataba wa makubaliano na mashirikiano (MoU) na nchi ya Msumbiji na Malawi lengo ikiwa ni kuunganisha nguvu za pamoja kulinda na kutunza vyanzo hivyo vya maji hasa katika mto Ruvuma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ,alisema kupitia mshirikiano hayo nchi hizo tatu zitaungana katika ulindaji na utunzanji wa vyanzo vya maji kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo ili waendelee kupata maji safi na salama.
“Nchi yetu ya Tanzania tumekuwa na mito mingi sasa baadhi ya mito unakuta inapita katika baadhi ya nchi zingine hivyo suala la ulindaji na utunzaji wa vyanzo vya maji lazima liwe endelevu”
“Faida yake ni kwamba mto ruvuma baina ya nchi hizi tatu tutaweka macho yetu katika ulindaji na utunzaji hivyo utakua na manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo katika kuhakikisha unakua endelevu na watanzania waendelee kupata maji safi na salama”
Aidha Waziri Aweso alisema kupitia mashirikiano hayo yatapelekea pia kuwepo kwa mikakati ya pamoja katika kuhakikisha kwamba wanapata manufaa ya uwepo wa mto Ruvuma.
Kadhalika, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kuwa ni moja ya chanzo kinachoathiri mito na baadhi ya vyanzo vya maji, Waziri Aweso aliwataka wadau wote kuungana kwa pamoja katika kulinda na kutunza vyanzo hivyo ili viweze kuwa endelevu na kuendana na kasi ta uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda
“Mkakati wa serikali juu ya kilimo cha umwagiliaji, tutafanyaje kilimo cha umwagiliaji kama hatuna vyanzo vya maji vya uhakika hivyo huu ni mkakati mahususi wa mhe. Rais wa kuhakikisha kwamba sisi kama Tanzania wenyewe na tuungane na nchi nyingine kuhakikisha kwamba masuala la ulindaji na utunzaji wa vyanzo vya maji inakua kipaumbele”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji-Wizara ya Maji na Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu ya Bonde la Mto Ruvuma, George Ligombela alisema Hati ya makubaliano hayo inawezesha ushirikiano wa nchi hizo tatu kuanzisha sekretarieti ya Bonde la mto Ruvuma itakayokuwepo katika mji wa Mtwara ambapo kutakuwa na watumishi kutoka nchi zote tatu.
Pia alisema kupitia mpango shirikishi wa usimamizi wa Rasilimali za maji katika bonde la Ruvuma, MoU hiyo imetilia mkazo katika kutekeleza kwa pamoja mashirikiano hayo.
“Sekretearieti hii lazima isimamiwe hivyo MOU hii imeanzisha kikao cha baraza la Mawaziri cha maanuzi katika Bonde hilo na kitapitia ajenda mbalimbali kuhusiana na mto Ruvuma, kutakuwa na kamati ya wataalamu itakayohusisha wakurugenzi kutoka Wizara zinazohusika na maji katika nchi zote tatu, lakini pia mabonde yaliyohusika,” alisema.
Pia alisema wataanzisha majukwaa ya wadau wa nchi zote ambayo yatahusisha wadau kutoka nchi ya Msumbiji, Malawi na Tanzania ili kujadili namna gani changamoto za usimamizi wa rasilimali za maji katika bonde hili limatatuliwa.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais