May 28, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Maendeleo ya Jamii yaja na vipaumbele vitano 2025/2026

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WIZARA ya Maendeleo ya Jamii,Wanawake na Makundi Maalum imeomba kiasi cha shilingi bilioni 76.05 ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa mwaka 2025/2026 huku ikitaja vipaumbele vitano itakavyovitekeleza katikia kipindi hicho.

Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/2026.Waziri wa Wizara hiyo Dkt.Dorothy Gwajima amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na kukuza ari ya jamii kushiriki katika kupanga na  kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoibuliwa katika  ngazi ya msingi. 

Ametaja vipaumbele vingine kuwa ni kuratibu na kuimarisha utoaji wa huduma za ustawi na maendeleo ya jamii ikiwa pamoja na kukuza  usawa wa kijinsia, kutokomeza vitendo vya ukatili,  uwezeshaji wanawake kiuchumi na upatikanaji wa  malezi bora katika familia na  kuimarisha mazingira ya ushiriki na mchango wa  Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya  Taifa.

Vile vile kutambua, kuratibu maendeleo na ustawi Makundi  Maalum wakiwemo watoto, wazee na  wafanyabiashara ndogondogo na kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia  katika Taasisi na Vyuo vya Ustawi na Maendeleo ya  Jamii.