January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Fedha kuanza kutekeleza maagizo ya rais kuhusu misamaha ya kodi

Na Josephine Majura,TimesMajira online, Dodoma

WIZARA ya Fedha na Mipango imepokea na kuanza kuyafanyia kazi maagizo ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, kuhusu misamaha ya kodi kwa fedha za misaada ili kutekeleza miradi ya vipaumbele.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini, Niinuma Takashi, ambaye alilalamikia suala la kodi kwa fedha za mikopo na misaada inayotolewa na nchi hiyo.

Waziri wa Fedha na Mipango,Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati wa kikao na Mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini Bw. Niinuma Takashi (hayupo pichani) ambapo alisema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ya Japan katika Nyanja mbalimbali, jijini Dodoma.

Dkt. Nchemba ameeleza kuwa Rais ametoa maagizo hayo kwasababu fedha za msaada zikitolewa kwa ajili ya kusaidia jamii na hata zikitozwa kodi pia kodi hiyo itatumika kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya nchi na wananchi kwa ujumla.

“Hili jambo tunalifanyia kazi na mpaka sasa tumeshaandaa waraka na tunasubiri ratiba ya Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kuupitisha katika baraza hilo ili ukidhi matakwa ya kisheria”, amesema Dkt. Nchemba.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto), akiteta jambo na Mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini Bw. Niinuma Takashi, baada ya Mkutano wao uliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

Amemuhakikishia Mwakilishi wa Balozi huyo kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Japan katika nyanja mbalimbali kwa maendeleo ya nchi zote mbili.

Naye Mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini Tanzania, Niinuma Takashi, aliahidi kuwa nchi yake iko tayari kuendeleza uhusiano na ushirikiano na Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kutoa misaada ya kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya vipaumbele ikiwemo bandari ya Kigoma na mradi wa maji Zanzibar.

Ujumbe kutoka Tanzania ukiongozwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa tano kulia) wakimsikiliza Mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini Bw. Niinuma Takashi (kushoto), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa endapo changamoto ya misamaha ya kodi itaondolewa kwenye fedha za misaada na mikopo inayotolewa, uhusiano wa Tanzania na wadau wa maendeleo utazidi kuimarika na kubainisha kuwa nchi yake ipo tayari kupokea maombi mapya ya kufadhili miradi mipya ya kipaumbele.