December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Elimu yaliomba Bunge kupitisha zaidi ya Trilioni moja bajeti ya mwaka 2024/25

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WIZARA ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia imeliomba Bunge kuidhinishiwa jumla ya Tsh.Trillioni Moja, Bilioni Mia tisa Sitini na Nane, Milioni mia mbili kumi na nane na elfu Mia tano na thelathini na nne (1,968,218,534,000.00.)
ya Makadirio ya Mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/ 2025.

Akisoma Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Bungeni leo Mei 7,2024  Waziri wa Wizara hiyo Prof.Adolf Mkenda amesema ili kuwezesha utekelezaji wa malengo kwa mwaka wa fedha 2024/25, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Fungu 46) inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,965,330,380,000.00 .

“kwa mchanganuo ufuatao shiliingi 637,287,706,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara ambapo Shilingi 585,225,031,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara na Shilingi 52,062,675,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 1,328,042,674,000.00 zinaombwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 1,033,393,669,000.00 ni fedha za ndani na Shilingi 294,649,005,000.00 fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

“Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO (Fungu 18) inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 2,882,154,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Mishahara ni Shilingi 1,319,040,000.00 na Matumizi Mengineyo ni Shilingi 1,563,114,000.00.

“Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa naomba sasa Bunge lako tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Bajeti ya Wizara (Fungu 46 na Fungu 18) yenye jumla ya Shilingi 1,968,212,534,000.00,”amesema Prof. Mkenda

Aidha amesema vipaumbe vya Wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2024/25,kuwa Wizara imepanga kutekeleza vipaumbele vitano vyenye lengo la kuongeza ubora wa elimu kwa kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata maarifa, ujuzi, kujiamini, kujiajiri na kuajirika.

Vilevile, vipaumbele vyenye kujielekeza katika kutegemeza tafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu katika agenda ya maendeleo ya nchi.

Ametaja vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/25 kuwa ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo nchini.

kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (amali na amali sanifu),kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu,kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na kuendeleza tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.