December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Elimu akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani)Prof.Joyce Ndalichako jana mkoani Dodoma

Wizara ya Elimu kukamilisha maandalizi ya somo la historia ya nchi ya Tanzania kwa shule ya msingi na sekondari

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema wizara hiyo inaendelea kukamilisha maandalizi ya  kuanza kufundisha somo jipya la historia ya Tanzania kuanzia Julai mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma  kufuatia agizo la Rais John Magufuli kutaka somo hilo lifundishwe nchini,Profesa Ndalichako amesema mpaka sasa tayari wizara hiyo imekamilisha kuandaa muhtasari kwa ajili ya somo hilo.

“Baada ya tamko la Rais kuhusiana na somo hilo kufundishwa mashuleni ,tulianza mara moja maandalizi ambapo mpaka sasa tumeshakamilisha zoezi la kuandaa mihtasari kwa ngazi zote.” amesema Profesa Ndalichako na kuongeza kuwa

“Hivi sasa vitabu vinaandaliwa kwa ajili ya kufundishia wanafunzi na tunatarajia hadi kufikia  Machi mosi vitabu vyote vitakuwa tayari na kwamba vitabu hivyo vinaandaliwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wabobevu katika historia  ya nchi ya Tanzania ili somo hilo jipya liweze kufundishwa kwa ufasaha mkubwa.”amesema

Profesa Ndalichako amesema,nchi ya Tanzania ina historia kubwa ambayo ikifundishwa kwa vijana nchini itasaidia kuwafanya wawe wazalendo na kulinda rasilimali za Taifa sambamba na kujua namna nchi ilivyopambana katika kujipatia uhuru.

“Somo hilo litafundishwa kwa lugha ya kiswahili kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita ili liweze kueleweka vizuri kwa wanafunzi .

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Leonard Akwilapo amesema kidato cha tatu ,cha  nne na kidato cha sita hawatafanyia mtihani mwaka huu isipokuwa wale wa kidato cha kwanza na cha  pili ndio watafanyia mtihani somo hilo.