December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Afya,yataja vipaumbele nane 2024

Na Penina Malundo

WIZARA ya Afya nchini imetaja vipaumbele vyake nane kwa mwaka 2024 ikiwemo suala la kuimarisha afua za kinga na utambuzi wa magonjwa mapema ilikuwawezesha wananchi kujikinga na magonjwa mbalimbali.

Pia imesema magonjwa yasioambukiza yanaonekana kushika kasi kwa tathimini walioifanya kwa mwaka 2023, inaonesha kati ya magonjwa 10 yanayoongoza kwa wagonjwa wa Nje (Opd),magonjwa hayo yanashika nafasi ya 10 kwa watoto chini ya miaka 5.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari kuhusu hali ya utoaji wa huduma ya afya kwa mwaka 2023 na vipaumbele vya wizara kwa mwaka  2024,alisema wizara iliweza kukaa na kufanya tathimini katika maeneo Matano ndani ya mwaka 2023 na kuja na vipaumbele hivyo vya kuhakikisha wanaboresha maeneo ambayo bado yapo nyuma.

Amesema wizara imejipanga kuanzisha huduma za watumishi wa afya ngazi ya jamii (CHW’s) na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na magonjwa yasiyo ambukiza (MYA).

Ummy amesema watahakikisha wanahimiza wananchi kubadili mtindo wa maisha ikiwemo kuzingatia ulaji unaofaa wa vyakula na kufanya mazoezi ili kuweza kupunguza magonjwa yasioambukizwa kuweza kuongezeka.

‘’Tumeona ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanavyozidi kushika kasi kama shinikizo la damu kutoka asilimia 2.7 hadi 5.6 kwa mwaka 2023,Ugonjwa wa kisukari idadi imeongezeka kutoka asilimia 1.6 hadi asilimia 2.5,hivyo wizara imekuja na mkakati kwa mwaka huu 2024 kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kufanya mazoezi,’’amesema na kuongeza

“Hivyo kutakuwa na program maalum ya kuhimiza watu kufanya mazoezi kwani asilimia kubwa ya magonjwa yasioambukiza yanasababishwa na tabia bwete na ulaji usiofaa Pamoja na watu kutofanya mazoezi,”amessema.

Amesema watu wanafanya mzaha na mafunzo ya Profesa Mohammed Janabi kuhusu masuala ya lishe, ambapo kwa asilimia kubwa yanasaidia kwani hata yeye ameanza kuyafuata na kuona yanamletea matokeo mazuri.

‘’Mafundisho ya Prof. Janabi yamekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakitupia picha ya pilau mtandaoni wakiambatanisha na maelezo ya Prof. Janab amekataza wakati mafunzo haya ni muhimu sana kwetu,’’amesema na kuongeza;

‘’Prof. Janabi amekuwa akisisitiza jamii kuepuka ulaji wa wanga ,matumizi ya sulari nyingi,chumvi nyingi na kusisitiza umuhimu kutokula vyakula vigumu nyakati za usiku,lakini watu wanafanya mzaha na mafundisho haya maana kunawakati hata mimi ananitisha na hapa mimi ni mwanafunzi wake tangu mei mwaka jana sinywi chai yenye sukari,amesema.

***Akizungumzia suala la Bima ya Afya

Ummy amesema serikali imeendelea kutoa huduma kwa wananchi katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuzingatia sera ya Afya ya mwaka 2007 inayotaka wananchi kuchangia gharama za afya.

Amesema katika mwaka 2023, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 85 ya wananchi wanapata huduma za afya kwa kulipia papo kwa papo kutoka mfukoni huku  asilimia 15 walikuwa wamejiunga na skimu mbalimbali za Bima ya Afya ikiwemo NHIF na bima binafsi.

Amesema kadri wananchi watakapojiunga kwa wingi katika bima ya afya ndipo gharama hiyo itaweza kupungua kwani lengo la huduma ya bima ya afya ni kuchangiana katika kutibiwa magonjwa.

Ummy amesema katika kila watanzania 100 ,watanzania nane tu ndio wanatumia bima za afya hivyo kilio cha bei ya bima kinaweza kushuka kulingana na watu wengi wakijiunga katika huduma hiyo.

Amesema kwa upande wa matibabu ya bure yapon a sera yake ipo ila utekelezaji wake ni hatua kwa hatua.‘’Serikali imeendelea kutekeleza sera ya huduma za afya bila malipo kwa makundi maalumu ambayo ni wajawazito, watoto wa umri chini ya miaka 5 na wazee wasio na uwezo hatua kwa hatua,’’alisema na kuongeza

‘’Katika mwaka 2022/23, kiasi cha shilingi bilioni 43.119 zilitumika kugharamia bidhaa za huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ikiwemo,Kiasi cha shilingi bilioni 30 zilitumika kununua, kusambaza na kutoa Chanjo kwa watoto walio chini ya miaka 5 ili kuwakinga na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kama vile Polio, kifaduro, donda koo, nimonia, tetanas, surau,Chanjo za wajawazito aina Tetanus Toxoid – TT iligharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.5 katika mwaka wa fedha wa 2022/23 pamoja na Dozi milioni 17.34 za dawa ya SP ili kukinga malaria kwa mjamzito na mtoto zilinunuliwa na kutolewa bure kwa wajawazito wote nchini ambapo shilingi  bilioni 7 zinatoka kila mwaka,’’amesema.