Na WAMJW-DOM,timesmajira,online
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imekabidhi vifaa vya kujikinga na UVIKO-19 kwa Mikoa 12 ya Tanzania Bara na Mitano ya Zanzibar vilivyotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kupitia shirika la Kimataifa ya Nutrition International (NI) ikiwa ni kuwakinga watoa huduma ya afya wakati wa kampeni ya utoaji wa huduma ya Matone ya Vitamini A nchini,
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa wawakilishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amesema vifaa hivyo vitaenda kuwasaidia watoa huduma za afya walio mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya nchini bila kuwasahau watoa huduma za afya ngazi ya jamii (CHW).
Dkt. Sichalwe amesema kutokana na changamoto ya UVIKO-19, Serikali inaendelea kuwapatia vifaa vya kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 watoa huduma waliopo katika vituo vya afya ili kuwawezesha kuendelea kutoa huduma za afya kwa ufanisi ikiwemo Kampeni ya utoaji wa Matone ya Vitamini A inayofahamika kama “Huduma ya Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto”.
“Vifaa hivi vimeanza kutolewa katika mikoa 12 ambayo ni Dodoma, Geita, Kagera, Morogoro, Katavi, Mwanza, Kilimanjaro, Shinyanga, Simiyu, Singida, Tabora na Tanga pamoja na Mikoa yote mitano ya Tanzania Visiwani. Ameongeza kuwa mikoa hiyo imechaguliwa kwa sababu ilikuwa na ufanisi duni katika utoaji wa hudumaza afya, hivyo kupitia msaada huu utasaidia kuimarisha kiwango cha ufanisi katika utoaji wa huduma za matone ya Vitamini A kwa watoto wengi zaidi” Alisema Dkt.Sichalwe.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Ray Masumo ameishukuru Serikali ya Canada kupitia Shirika lake la Nutrition International kwa kuendelea kuiunga mkono serikali katika vita dhidi ya UVIKO-19 na changamoto nyingine za Kilishe.
Dkt. Masumo amesema vifaa hivi vitawasaidia watoa huduma ya afya waliopo mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya ikiwemo Huduma ya mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto kwani malengo yaliyopo ni kuhakikisha ifikapo Mwaka 2025 watoto wote nchini wafikiwe na huduma ya matone ya Vitamini A kupitia vituo vya afya vilivyopo nchini.
Nae Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Nutrition International Dkt. Daniel Nyagawa amesema wamechukua uamuzi wa kutoa vifaa kwa Serikali ikiwa kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazochukuliwa katika kupambana na UVIKO-19 na wataendelea kushirikiana na afua nyingine ikiwemo zile za Kilishe ambazo shirika hilo limekuwa likizitekeleza hapa nchini.
Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mkurugenzi wa huduma za Afya Dkt. Mwanahamisi Hassan amesema vifaa hivyo vitawasaidia watoa huduma za afya waliopo mstari mbele katika vita ya UVIKO-19 hivyo anawakaribisha wadau wengine kujitokeza katika kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali katika Vita hiyo.
Jumla ya Katoni 6000 za Barakoa (Mask) na Vitakasa Mikono (Sanitizer) lita 6000 vyenye gharama ya Milioni 57 ambavyo visambazwa katika mikoa 17 ikiwemo 12 ya Tanzania bara na 5 ya Tanzania visiwani.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria