December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara kuanzisha leseni ndogo uchenjuaji madini

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam.

WIZARA ya Madini imethibitisha kuanzishwa kwa leseni ndogo za uchenjuaji wa madini, ili kuepusha uchenjuaji holela ambao umebainika kufanywa na wachimba madini.

Akitoa ufafanuzi juu ya jambo hilo mapema leo katika ufunguzi wa kikao cha siku tatu kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko, amesema wameamua kuanzisha leseni hizo ili kuepusha ujengwaji wa mialo kiholela, ambayo ilikuwa ikijengwa hata katika makazi ya watu.

Dkt.,Biteko katika kikao hicho, amepokea maoni mbalimbali ya wadau wa sekta ya madini nchini yasaidie katika urekebishaji wa sheria ya madini sura namba 123 na kanuni zake ili kuboresha shughuli za sekta ya madini.

“Mbali na hayo yote, tumeamua kutoka ofisini kuja kuwasikiliza wadau wa sekta hii ili mtoe mapendekezo yenu yatakayosaidia kurekebisha sheria ya madini sura namba 123 na kanuni zake, ili kuboresha utekelezaji wa shughuli za sekta yetu,” amesema Dkt. Biteko.

Pia ametaja maeneo ambayo yanatakiwa kuboreshwa ni pamoja na kanuni ya masoko, kanuni ya eneo tengefu la Mererani na kanuni ya uongezaji thamani madini, ili kuboresha shughuli za sekta ya madini na kurejesha minada ya madini ya vito.