July 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara Katiba yapokea Tuzo maonesho ya Sabasaba



Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

MKURUGENZI Msaidizi wa Sehemu ya Utatuzi wa Migogoro, Wizara ya Katiba na Sheria, Felix Chakila, amesema wizara imefanikiwa kuwahudumia wananchi 2,008 katika kipindi chote cha Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), mafanikio yaliyochangia kutwaa tuzo katika maadhimisho hayo yaliyohitimishwa Julai 13, 2026 chini ya mgeni rasmi, Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.


Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Chakila alisema ushiriki wa wizara katika maonesho hayo umeiwezesha kusogeza huduma za sheria karibu zaidi na wananchi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa Serikali wa kuhakikisha haki na huduma za kisheria zinawafikia Watanzania kwa urahisi.


Alisema licha ya huduma hizo kutolewa bila malipo kwa wananchi katika maonesho hayo, ziliwezekana kutokana na uwekezaji wa Serikali unaolenga kuboresha upatikanaji wa haki na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya kisheria.


“Tulifanikiwa kuwahudumia wananchi takribani 2,008 waliofika katika banda letu. Hii ni fursa muhimu ya kurudisha huduma kwa jamii na kutekeleza wajibu wetu kama wizara na Serikali kwa ujumla,” alisema Chakila.


Aliongeza kuwa uzoefu walioupata katika maonesho ya mwaka huu utasaidia kuboresha maandalizi ya ushiriki wa mwakani, huku akibainisha kuwa bado kuna mahitaji makubwa ya huduma za sheria kutoka kwa wananchi.


Chakila alisema idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza ilionesha wazi umuhimu wa kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya haki, kwani muda wa maonesho haukutosha kuwahudumia wananchi wote waliohitaji huduma.


Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na taasisi nyingine za haki ili kupata ushauri na huduma za kisheria kwa wakati, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta hiyo utaongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.