Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema wizara hiyo imejiwekea vipaumbele 10 inavyotarajia kuvitekeleza katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 kwa lengo la kuboresha huduma za afya nchini.
Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipokuwa akiwasilisha hotuba ya mapato,makadirio ya matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Ametaja vipaumbele hivyo ni pamoja na Kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa,Kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa na vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Taifa, Kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini.
Vipaumbele vingine ni Kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga, Kuimarisha upatikanaji na uendelezaji wa wataalam katika Sekta ya Afya kwa fani za kati,ubingwa na ubingwa bobezi, Kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi nchini,
Kuendeleza na kusimamia afua za Tiba Asili na Tiba Mbadala.
“Lakini pia Kuimarisha upatikanaji wa huduma za magonjwa ya kuambukiza, magonjwa
yasiyoambukiza na magonjwa ya mlipuko,Kuimarisha huduma za afya ya akili, huduma za utengamao hususan kwa watoto, wazee na watu wenye ulemavu na Kusimamia Tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya,”amesema Waziri Ummy
Kadhalika amesema kuwa Kwa mwaka 2024/25, Wizara imekadiria kutumia kiasi cha Shilingi 1,311,837,466,000 kutekeleza vipaumbele hivyo kwa kutumia afua 89 katika Kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa ambapo kiasi cha Shilingi 117,611,588,304.00 kimetengwa zitakazotekeleza afua mbalimbali.
Ametaja afua hizo ni pamoja na Kuendelea kuimarisha utekelezaji wa afua za chanjo kwa kuwafikia watoto 3,117,564 wenye umri chini ya miaka miwili (2), wasichana 871,429 wenye umri wa miaka tisa (9) na wajawazito 3,298,437 (Shilingi 115,369,238,904.00) na kutekeleza afua za lishe ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhimiza unyonyeshaji na ulishaji sahihi wa watoto.
Amesema afua nyingine ni elimu ya lishe kwa jamii na kuimarisha Mpango wa kuongeza virutubishi kwenye vyakula ambapo ununuzi na usimikaji wa mashine 300 za kuongeza virutubishi (Dozifiers)utafanyika (Shilingi 1,607,700,000.00) na kimarisha utekelezaji wa afua za usafi na afya mazingira katika jamii, Mipakani, taasisi za umma na binafsi ikiwemo kutekeleza kampeni ya mtu ni afya awamu ya pili.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria