Judith Ferdinand, Mwanza
Wito umetolewa kwa jamii kuto nyamazia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo vipigo kwa wanawake, kujihusisha kimapenzi na wanafunzi, mimba na ndoa za mapema.
Huku waendesha bodaboda wakitakiwa kujiepusha na kutojihusisha kimapenzi na wanafunzi wa kike kwani kumekuwepo na madai ya wao kuwashawishi kwa kuwapa lifti wakati walienda au kutoka shule.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Magu iliopo mkoani Mwanza, Salum Kalli wakati akizindua kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambayo huadhimishwa kila mwaka Novemba 25 hadi Disemba 10.
Ambapo lengo la kampeni hiyo ni kuwaleta pamoja wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali kuhamasisha jamii kujiepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika wilayani Magu ukiratibiwa na Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI lenye makazi yake Nyamhongolo jijini Mwanza ambalo limekuwa likitoa elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ikewemo Magu mkoani Mwanza.
Kalli amesema jamii haipaswi kunyamazia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo vipigo kwa wanawake, kujihusisha kimapenzi na wanafunzi, mimba na ndoa za mapema.
Pia amewahasa bodaboda kuwa mabalozi wa kuwalinda watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao na wajiepushe kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wa kike kutokana na kudaiwa kwamba wamekuwa wakiwashawishi kuwapa lifti wakati wa kwenda ama kutosha shule.
Sanjari na hayo Kalli amesema Rais Samia Suluhu Hassan amewaletea kiasi cha fedha cha bilioni 2.46 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 123 vya madarasa katika shule za sekondari.
“Tusipowalinda wanafunzi mnataka akasome nani kwenye hayo madarasa,tushirikiane ili tuhakikishe wanatimiza ndoto zao,” amesema Kalli.
Mbali na hayo,pia amewaonya baadhi ya watendaji katika vyombo vya utoaji maamuzi kuchelewesha kesi zinazohusiana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo mimba kwa wanafunzi wa kike kwa kisingizio cha upelelezi kutokamilika na kusababisha kesi hizo kutopata mafanikio.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally amesema katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mwaka 2021, shirika hilo litaendesha shughuli mbalimbali ikiwemo makongamano na midahalo ili kuendelea kuhamasisha jamii kupinga na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Hata hivyo takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa Mwanza kitengo cha Dawati la Jinsia zimebainisha kuwa kesi 84 za ukatili wa kijinsia kwa mwaka 2020 zilipata mafanikio huku kesi 48 zikipata mafanikio kwa mwaka 2021 kuanzia mwezi Januari hadi Novemba na hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wahusika.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam