December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Habibu Makusanya (mwenye miwani) akiwaongoza waumini wa Kiislamu katika msikiti mkuu wa Ijumaa mjini Shinyanga kusoma dua maalumu kwa ajili ya kumuomba Mwenyezi Mungu aondoe ugonjwa hatari wa COVID - 19 (Picha na Suleiman Abeid, Timesmajira)

Wito maombi ya JPM waanza kwa kishindo

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

WAUMINI wa Kiislamu mjini Shinyanga wametekeleza agizo lililotolewa na Rais John Magufuli kwa kuomba dua maalumu ili kumuomba Mwenyenzi Mungu aweze kuwaondolea Watanzania ugonjwa wa corona ambao umesababisha maelfu ya vifo katika mataifa mbalimbali duniani.

Maombi hayo yalifanyika jana katika misikiti ya mjini Shinyanga, ambapo waumini hao waliendesha dua maalumu mara baada ya Sala ya Ijumaa.

Juzi Rais Magufuli alitoa wito kwa Watanzani kila mmoja kwa imani yake kufanya sala ili kumuomba Mungu atuepushe na janga la corona, Walimshukuru Rais Magufuli kwa kusimamia msimamo wake wa kutofunga nyumba za ibada.

Katika maombi hayo waumini hao walisema ni vyema kila Mtanzania akafanya toba ya dhati na kuacha kufanya matendo maovu yanayomchukiza mwenyezi Mungu na hivyo kusababisha atoe adhabu yake kupitia ugonjwa hatari wa corona.

Akiongoza dua hiyo katika msikiti mkuu wa Ijumaa mjini Shinyanga, Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Habibu Makusanya alisema kitendo cha Rais Magufuli kutangaza siku tatu kwa ajili ya maombi maalumu kwa madhehebu yote ya dini hapa nchini kinastahili kupongezwa na kwamba huenda Mungu akapokea maombi hayo na kuondoa ugonjwa huo.

“Tunampongeza Rais wetu kwa uamuzi wake wa busara, kwa kweli amekaa na kutafakari kwamba, suluhisho la ugonjwa huu ambao umeteketekeza maelfu ya binadamu hapa duniani ni kurejea kwa Mwenyezi Mungu, yeye ndiye muweza wa kila jambo,”

“Lakini pia hatuna budi kumshukuru kwa uamuzi na msimamo wake wa kutofunga nyumba za ibada  na badala yake amehimiza suala la watu kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu hatari, ni juu yetu kuhakikisha tunachukua kila tahadhari na kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima,” alisema Shekhe Ismail.

Kwa upande wake Sheikh wa Msikiti wa Mufti Issa Shaaban Simba uliopo majengo mjini Shinyanga, Balulisa Khamis aliwataka waumini wa Kiislamu kwa ujumla kumrejea Mungu na kujiepusha kufanya maasi mbalimbali ambayo ni chukizo mbele zake Mungu.

“Sisi sote lazima turejee kwa Mungu kwa kuleta toba ya kweli na kujiepusha na maasi, lakini pia tutumie fursa iliyotolewa na  Rais ya kutofunga nyumba za ibada kwa kuzingatia maelekezo yote yanayotolewa

kuhusu kujikinga na ugonjwa huu,” alisema na kuongeza;

“Rais wetu ameonesha jinsi gani anavyoheshimu dini zetu, pamoja na ushauri wa watu wengine kwamba atoe tamko la kufunga nyumba za ibada yeye amekataa na kusema Mungu ndiye pekee anayepaswa kuombwa wakati wote, na hata juzi ametumia aya za Kur-an kuonesha kwamba tunapomkosea

Mungu lazima atupe mitihani na majaribu, sasa tujeree kwake,” alieleza Balulisa.