Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Wito umetolewa kwa jamii kuachana na imani potofu juu ya chanjo mbalimbali ikiwemo ya Polio zinazotolewa kwa ajili ya kuwakinga watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na maradhi.
Badala yake wametakiwa kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hizo ili ziweze kuwakinga na maradhi mbalimbali kama vile kupooza ambao unasababishwa na polio.
Ambapo serikali imekuwa na utaratibu wa utoaji chanjo kila siku katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kukinga magonjwa mbalimbali kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mwanza Amos Kiteleja,wakati akizungumza na Majira ofisini kwake mkoani hapa, amesema chanjo hizo zinawasaidia watoto katika maisha yao kwani watoto wadogo ndio wanaathiriwa sana na magonjwa ya mlipuko.
Kiteleja amewaomba wazazi,walezi na jamii wenye watoto waliochini ya umri wa miaka mitano wahakikishe wanapata chanjo ya polio kwa njia ya matone na chanjo nyingine zote huku wakiachana na mila na imani potofu juu ya chanjo hizo kwani ni salama na hazina madhara.
“Kama ugonjwa wa kuharisha, polio,pepo punda,kifadulo,surua na magonjwa mengine ambayo katika nchi yetu ya Tanzania watoto hawa chini ya umri wa miaka mitano tunawakinga ili wasiweze kudhurika na magonjwa kwaio ndio maana hivi karibuni tutatoa chanjo ya polio kwa njia ya kampeni,” amesema Kiteleja.
Amesema kama nchi kila siku ina utaratibu wa kutoa chanjo katika vituo vyao vya huduma na kama kunakuwa na tishio la ugonjwa uwa wanatoa chanjo kwa njia ya kampeni ambazo wanaweza kufanya kituoni ama kupita nyumba kwa nyumba.
Pia amesema,hivi karibuni kutokana na tishio la ugonjwa wa polio katika nchi jirani watafanya kampeni ya nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha kwamba wanawafikia watoto wote ambapo wamekadiria kufikia watoto zaidi ya 800,000.
“Haijalishi ameisha pata chanjo hapo nyuma au hajapata kabisa ata kama amezaliwa leo wote watapewa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa polio ambayo itatolewa kwa njia ya matone kupitia mdomoni,”
Vile vile amesema,magonjwa yote ambayo wanayazuia kwa watoto ni hatari mfano ugonjwa wa surua ukitokea watoto wengi wanaweza kuathirika na kufa hivyo kupata hasara katika taifa kadhalika polio watoto wengi wataugua utaenda mpaka kwa watu wazima wataugua,watapata ulemavu na wengine watakufa hivyo kuleta shida kubwa katika taifa.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa utoaji wa chanjo hizo zinamanufaa katika nchi ikiwemo watoto wanaozaliwa wanaishi na kuwa watu wazima na kufanya shughuli za uzalishaji katika taifa na kuwa na taifa lenye uchumi kwani watakuwa ni nguvu kazi ya taifa lenye afya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza Dkt.Pima Sebastian, amesema watakuwa na zoezi la utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto zaidi ya 92,000, ambayo itasaidia watoto wasipate ugonjwa wa kupooza unaoletwa na virusi vya polio.
Amesema,mila na imani potofu ni kitu kinachowarudisha nyuma hivyo wananchi wazipuuze na kuwapeleka watoto waweze kapatiwa chanjo.
“Sisi tunaamini watoto wote wakipata chanjo tunaweza kuzuia watoto,taifa la Leo na kesho wasiweze kupooza na kuwa na taifa lenye wananchi wenye afya bora ambao wanaweza kutumika kama nguvu kazi ya kujenga nchi,hivyo wazazi wahakikishe watoto wote wanapata chanjo,” amesema Dkt.Pima.
Mmoja wa wananchi wa jijini Mwanza ambaye amempeleka mtoto wake kupata chanjo katika kituo cha Afya Makongoro,Maria Muna,amesema mtoto wake anapata huduma ya chanjo kwa mara ya tatu ambapo umuhimu wa chanjo ni kuwasaidia watoto wasipate magonjwa mbalimbali ikiwemo wa kupooza
Hivyo ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi wengine kuwapeleka watoto wao waweze kupata huduma ya chanjo ili kuepuka kupata magonjwa kwani ni muhimu na zinamafaa sana maana unaweza kukuta ametumia lakini bila dawa ukakuta kidonda kimepona kumbe ni zile chanjo alizopata zinafanya kazi.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best