December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wilaya ya Ilala yajivunia kutekeleza miradi kwa asilimia 99



Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar es Salaam.

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Ilala, Said Side, amepokea Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwezi Januari hadi Juni mwaka huu, kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM katika wilaya hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho mbele ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu Wilaya ya Ilala, wakati wa upokeaji wa taarifa hiyo, Mwenyekiti huyo amesema, viongozi wa CCM katika wilaya hiyo wamekuwa shuhuda, baada ya kufanya ziara na kukagua miradi mbalimbali inayosimamiwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala na kuona imetekelezwa kwa asilimia 99.

Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi hicho cha miezi sita kwa mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, amempongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kiasi cha fedha zaidi ya bil.15 ambazo zimeelekezwa upande wa elimu kupitia katika Manispaa ya Ilala.

Ametaja miradi mingine ambayo tayari imekamilika katika Wilaya hiyo, kuwa ni pamoja na Miundombinu ya Barabara, Elimu, Afya na huduma ya maji safi na salama.

Pia amesema kuwa, Serikali ya awamu ya Sita imetoka zaidi ya bilioni moja ambazo zimekwenda kutumika kwenye usimamizi wa mitihani ya kitaifa kuanzia elimu ya Msingi na Sekondari.

Ajizungumzia Sekta ya Afya, amesema taarifa ya utekelezaji wa ilani hiyo imetekelezwa kwa kiasi kikubwa katika ujenzi na usimamizi wa vituo vya afya na zahanati mbalimbali zilizopo kwenye wilaya hiyo na kufanya wananchi kwasasa kupata huduma bora za afya pindi wanapokwenda kupatiwa matibabu.

“Nimpongeze Mwenyekiti wetu CCM Taifa kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya kwa wananchi wake hususan wana Ilala kwa kipindi Cha miezi sita tumeweza kutekeleza Ilani ya chama katika kukamilisha miradi mbalimbali kwa asilimia 99,”amesema Mpogolo.

Aidha Mpogolo ameeleza kuwa wilaya ya Ilala Ina jumla ya wakazi wengi, huku akitaja miradi mkakati iliyopo kuwa 131, huku akidai kuwa hilo ni jambo jema na la kujivunia kwa fedha hizo kutolewa na kusimamiwa kwa miradi hiyo na kukamilika.

Ameongeza kuwa, kuna miradi ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika, inaendelea kutekelezwa, ambapo amewataka wananchi kwa ujumla kuendelee kuwa na imani na Serikali ya awamu ya Sita.