Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi.
Jamii imetakiwa kuchangamkia fursa ya kupata mafunzo wezeshi ya kutumia teknolojia kwenye kazi mbalimbali kama njia ya kukabiliana na mabadiliko ya utendaji kazi yatakayoboresha ufanisi na kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mwanamvua Mrindoko amesema hayo leo katika viwanja wa CCM Azimio Manispaa ya Mpanda mkoani humo wakati wa maenesho ya teknolojia mbalimbali na bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali ambayo yameanza kufanyika Oktoba 25 hadi Oktoba 31 mwaka huu.
Maonesho hayo yanayoenda kwa jina la Wiki ya Mwanakatavi yenye kauli mbiu isemayo “Katavi yetu talii,wekeza,imarisha uchumi kwa maendeleo endelevu” yamelenga kuhuwisha upatikanaji wa fursa za kiuchumi kupitia sekta za kilimo,mifungo,uvuvi,utalii pamoja na kukuza matumizi ya teknolojia kwenye sekta hizo.
Mrindoko amesema kuwa serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wananchi wa ndani na nje ya mkoa huo hususani wanawake na wasichana ambao wamekuwa nyuma kwenye matumizi ya teknolojia ili waweze kuvutiwa zaidi kujifunza na kutumia teknolojia ambayo itarahisisha katika shughuli za kila siku.
“Uzoefu uonanyesha kuwa wanawake na wasichana wengi kwa idadi ni wajasiriamali na wahudhuriaji kwenye maonesho, nitumie fursa hii kuwasihi kuondoa hofu ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwenye utendaji wa kazi naamini kupitia wiki ya Mwanakatavi ni jukwaa bora zaidi la kujifunza kwa njia ya kubadilishana uzoefu na wanawake na wanaume wengine ambao tayari wameingia kwenye matumizi ya teknolojia,”amesema.
Mkuu wa Mkoa huyo amefafanua kuwa “Teknolojia imegunduliwa ili kuchochea mapinduzi ya kiuchumi wanawake na wasichana na jamii yote bila kujali jinsi njooni kwenye wiki ya Mwanakatavi mjifunze na muone fursa kubwa ambazo zitawasaidia kuimarika zaidi,,”amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe, Shamimu Mwariko amesema serikali inaendelea kuhamasisha masuala ya usawa wa kijisia kwa kuwajengea uwezo wanaume kutambua umuhimu wa wanawake na wasichana kushirikishwa kwenye masuala ya uchumi kuanzia ngazi ya familia.
Huku wanaume kugatua mamlaka na kumpa mwanamke uwezo wa kuendesha mitambo ya teknolojia kwenye sekta ya kilimo na zingine nyingi.
“Wiki iliyopita tulikuwa na wiki ya wanawake vijijini ambayo ilijenga kujenga uelewa na uwezo wa wanawake kutambua fursa zilizopo kwenye maeneo yao,kuweka mazigira wezeshi kwa kutambua fursa zilizopo za umilki wa ardhi pamoja na sio tu kuwa na uwezo wa kuendesha mitambo ya teknolojia bali kumilki teknolojia hizo,”amesema Shamimu.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa ni wakati muafaka wanawake na wasichana wa vijiji ambao wako nyuma licha ya hamasa mbalimbali kupatiwa na mazingira wezeshi wanapaswa kuamka kwenye kutafuta fursa na jamii iko tayari kuwapokea na kuwatia moyo kuinua uchumi wao.
Ofisa Kilimo wa Bodi ya Pamba Mkoa wa Katavi Filbert Bugelaha amesema maonesho ya wiki ya Mwanakatavi ni jukwaa kubwa ambalo wanalitumia kama sehemu ya kufanya mdahalo na wadau mbalimbali wa kilimo kuhamasisha jamii ya wakulima kuzingatia matumizi ya teknolojia ili kukuza uzalishaji wa zao la pamba.
Amefafanua kuwa teknolojia haikwepeki kwa hali ya mwelekeo wa dunia kwani ili jamii iweze kufikia uzalishaji mkubwa inapaswa kutokuogopa kuitumia teknolojia.
” Tumekuja kwenye maonesho haya na teknolojia bora zaidi ya umwagiliaji ya viuatilifu shambani ya pamba inayoitwa drone au ndege inayoendeshwa bila rubani inauwezo mkubwa wa kumwagilia shamba dawa la ukubwa wa hekari nne kwa muda mfupi zaidi,”amesema Bugelaha.
Nao baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Katavi akiwemo Sara Jackson ameishukuru serikali ya mkoa kwa kuanzisha maonesho hayo ambayo wanayatumia kama sehemu ya darasa la kujifunzia namna bora ya kukuza biashara zao.
Sara amesema kuwa wananchi wengi hukosa maonesho ya kilimo ya nane nane ambayo hufanyika kila mwaka kikanda mkoani Mbeya kwa sababu ya gharama kubwa ambazo wanashindwa kumundu.
Hivyo kusogezewa kwa maonesha ya namna hiyo ni hatua kubwa ya kutengeneza mazingira wezeshi kwa wananchi kujikwamua kiuchumi.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi