Na Penina Malundo
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy
Mwalimu, amesema kuanzia Jumatatu, wiki ijayo hadi wiki mbili zijazo
ndipo Tanzania itakuwa imepata mwelekeo halisi wa maambukizi ya Corona
hapa nchini.
Waziri Ummy aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa viongozi
wa madhehebu ya dini ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la
World Vision uliolenga kuelimisha jamii dhidi ya ugonjwa wa Corona.
“Kuanzia Jumatatu hadi wiki mbili zijazo ndipo tutajua kama tutalala
au hatutalala,” alisema Ummy bila kuingia kwa undani zaidi.
Waziri Ummy alisema Tanzania imeanza kupata maambukizi ya Virusi vya
Corona ya ndani kuanzia maambukizi yaliyopatika Aprili 8, mwaka huu.
Alisema hivi sasa tumetoka katika maambukizi ya mlipuko wa ugonjwa
virusi ya Corona yanayoletwa kutoka nje na imeingia kwenye maambukizi
ya ndani kwa ndani.
“Ugonjwa tumeletewa kutoka nje, hivi sasa takwimu za jana, juzi na
wiki iliyopita tumeanza kuambukizana wenyewe kwa wenyewe. Ili viongozi
wangu wa dini naomba niliweke wazi.
Ndani ya siku chache tutaingia katika community transmission. Maana
yake tutapata mgonjwa ambaye hajui ugonjwa ameupata wapi? Sasa hivi
amekuja mtu anamuambikiza fulani ndio maana tunafanya contact kujua.”
Alifafanua kuwa hatua ya maambukizi katika jamii ni ngumu kujua
aliyeambukizwa amepewa na nani na kwamba ndani ya siku chache
inawezekana tukaingia katika hatua hiyo.
Alisema kuwa tahadhari kubwa inahitajika ili kuzuia kuendelea kwa
maambukizi ya kijamii itasababisha kuongezekana kwa kasi ya maambukizi
katika jamii.
Alisema kwa sasa kwa jinsi hali ya maambukizi ya Corona ilivyo nchini
ni jambo la kumshuruku Mungu. Alisema takwimu za Shirika la Afya
Duniani (WHO) zinaonesha duniani kuna wagonjwa wa COVID 19 milioni 1.3
na kwa Afrika kulingana na takwimu za Kituo cha Kudhibiti Magonjwa
Afrika kuna wagonjwa 10,000 na vifo 500.
Alisema kutokana na takwimu hizo sisi kama Tanzania hatuwezi kuwa na
kinga ya kutopata ugonjwa huu, lakini tunamshukuru Mungu kwa sababu
hali bado sio mbaya.
“Tupo hapa kwa ajili ya Mungu, kwa sababu wakati mwingine inapita siku
mbili hadi tatu bila kupata negative (mwenye maambukizi), Mungu
anasikiliza sala zetu, kwani WHO walikuwa wametukadiria kwamba
tutakapofika Aprili katikati tutakuwa na wagonjwa 1,000 na
tutakapofika Mei katikati tutakuwa na wagonjwa 10,000,” alisema Ummy
na kuongeza;
“Hayo ndiyo yalikuwa makisio ya WHO, kwa hiyo hadi sasa hivi
tumesharuka kiunzi cha WHO tangu tumetangaza mgonjwa wa kwanza Machi
16, mwaka huu hadi leo ni wagonjwa 25.
Kwa hiyo tuna kila sababu ya kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu.”
Aliendelea kuwataka viongozi wa dini kuendelea kuhimiza wananchi
wazidi kuchukua hatua za kujikinga na COVID 19.
Alisema ndani ya siku mbili tatu watatoa mwongozo kwamba mtu akitoka
ndani ya nyumba yake avae barakoa (mask) au atakapoenda sehemu ya
watu wengi, hivyo viongozi wa dini waendelee kuhamasisha jamii
utekelezaji wa maelekezo ya kukabili COVID 19.
“Serikali itatangaza hivi karibuni wananchi kuchukua tahadhari, kwani
tafiti zinaonesha virusi vya Corona vinaweza kusambaa na kuambukizwa
kwa njia ya hewa hivyo maelekezo ya kutumia barakoa yatatolewa ili
kuondokana na maambukizi,”alisema na kuongeza;.
“Tafiti zimeonesha kuna uwezekano wa Virusi vya Corona vinaweza
kuenezwa kwa njia ya hewa hivyo tutaleta muongozo wa kuanza kutumia
Barakoa (Mask) kwa jamii ili kuziua maambukizi kuenena kwa njia ya
hewa” alisema
Alisema waumini wenye dalili za kukohoa, kifua na homa wabaki
nyumbani na kuzuia mikusanyiko na misongamano isiyokuwa ya lazima.
Waziri huyo alisema ni wajibu wa kila kiongozi wa dini kuhakikisha
wanaendesha ibada katika utaratibu na mazingira yasiyo hatarishi ili
kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.
Alifafanua kuwa makongamano ya dini sio muhimu kwa wakati huu. Ummy
aliwataka viongozi hao wa madhehebu ya dini kuendelea kufanya ibada
katika mazingira ya usalama kati yao na waumini sambamba na
kuwahamasisha waumini kuepukana na vitendo vya kushikana na
kukumbatiana.
“Tunaomba pia ibada ifanyike muda mfupi, pia wekeni utaratibu wa
kupunguza msongamano wa waumini wakati wa kuingia na kutoka katika
nyumba za ibada,” amesema Ummy.
Waziri Ummy alisema katika kipindi hiki cha sikukuu kuna watu watatoka
mijini kwenda vijijini. “Tujiulize kama kuna ulazima wa watu kutoka
mijini kwenda vijijini. Tusije tukawapelekea wazee wetu magonjwa hasa
kulingana na mlipuko wa ugonjwa huu hususani Dar es Salaam, je una
haja ya kwenda kijijini?”Alihoji Waziri Ummy na kusisitiza;
“Tunaenda kuwapelekea ugonjwa wazee wetu. Sisi tunashauri kama kuna
mtu anaweza kujizuia kutoenda kwa wazazi, tunamshauri abaki mjini.”
Alisema shule zimefungwa ili watoto wakae nyumbani katika sehemu
salama, lakini wanazurura mitaani. “Hiki sio kipindi cha watoto
kuzurura,”alisema. Alisisitiza kwamba dhamira ya Serikali kufunga
shule na vyuo ni kuwawezesha watoto wakae katika mazingira sahihi,”
alisema.
Awali Mkurugenzi wa World Vision Tanzania, Gilbert Kamanga, alisema
shirika hilo lipo bega kwa bega kushirikiana na Serikali katika
mapambano dhidi ya ugonjwa virusi vya Corona.
Aliwataka viongozi wa dini kutoa ujumbe sahihi kuhusu Corona akisema
ni miongoni mwa watu wanaoaminika katika jamii pamoja na kufuata yale
yanayoelekezwa na Serikali kuhusu ugonjwa huo.
“Tushikane mkono pamoja tupambane na ugonjwa huu wa corona. World
Vision ipo tayari kushirikiana na Serikali katika mapambano haya na
kuweka mikakati,” alisema Kamanga.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa