January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WHO : Dawa ya Trump haina uwezo wa kutibu Corona

GENEVA, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema limesitisha majaribio ya dawa aina ya hydroxy-chloroquine kwa wagonjwa wanaougua virusi vya corona.

Rais wa Marekani Donald Trump alisisitiza dawa hiyo ni muhimu na imekuwa ikitibu virusi vya corona vinavyosababisha COVID-19

Hatua hiyo inafikiwa baada ya ripoti kuwa, dawa hiyo inayotibu malaria inaongeza vifo miongoni mwa wagonjwa wa corona. Awali, Rais wa Marekani Donald Trump alisisitiza dawa hiyo ni muhimu na imekuwa ikitibu, kwani hata yeye mara nyingi amekuwa akiitumia.

Majaribio hayo yalikuwa sehemu ya mshikamano wa kimataifa unaoongozwa na WHO katika juhudi za kutafuta tiba dhidi ya virusi vya corona, kutokana na madawa yaliyotengenezwa kutibu malaria, ukimwi na kifua kikuu.

Hivi karibuni wanasayansi wa Marekani na Uswisi waliripoti kupitia jarida maarufu la kitabibu la The Lancet, kwamba hydroxy-chloroquine na madawa mengine ya aina yake yanaweza kuzidisha hatari ya kufa mgonjwa wa COVID-19 na kuharakisha kasi ya mapigo ya moyo.

Pia wanasayansi hao waliongeza kuwa, hawakubaini ufanisi wowote wa dawa hizo katika kutibu wagonjwa wa virusi vya corona. Mkurugenzi Mtendaji wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, shirika hilo sasa linachunguza data za usalama wa dawa hizo.

Mbali na hayo, Ofisi ya Kansela wa Ujerumani inaazimia kurefusha kipindi cha masharti ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona Julai 5,mwaka huu wakati huo huo ikiendeleza hatua za kulegeza baadhi ya vikwazo.
Hayo ni kwa mujibu wa rasimu ya maazimio ya mazungumzo baina ya wakuu wa majimbo yanayounda shirikisho la Ujerumani, iliyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari.

Kwa mujibu wa rasimu hiyo, kwa sasa watu hadi 10 au watu wa familia mbili, wataruhusiwa kujumuika mahali pamoja.

Baada ya muda wa mwisho wa masharti yanayoheshimiwa kwa wakati huu ambao ni Juni 5,mwaka huu wakazi wa Ujerumani watatakiwa kuendelea kuacha angalau umbali wa mita 1.5 kati ya mtu mmoja na mwingine, na kuendela kuva barakoa zinazofunika mdomo na pua.

Katika hatua nyingine,WHO linasema ingawa Afrika ndilo eneo ambalo lina idadi ndogo zaidi ya waathirika wa ugonjwa wa COVID-19, lakini kuna wasi wasi kuwa ugonjwa huo utaenea kimya kimya iwapo viongozi wa bara hilo hawatalipa umuhimu suala la vipimo.

Mjumbe wa WHO, Samba Sow ametahadharisha kuwa, ukosefu wa vipimo huenda ukapelekea janga la COVID-19 kuenea kimya kimya barani Afrika na hivyo viongozi wa bara hilo wanapaswa kulipa kipaumbele suala la vipimo.

Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC), hadi kufikia Mei 26, idadi ya waliofariki kutokana na COVID-19 barani Afrika walikuwa ni 3,471.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliofariki ni rais wa zamani wa Jamhuri ya Congo, Jacques Joachim Yhombi-Opango na Waziri Mkuu wa zamani wa Somalia, Nur Hassan Hussein.

Aidha, kwa mujibu wa takwimu hizo idadi ya walioambukizwa COVID-19 barani Afrika ni 115,346 huku 46,426 wakipona baada ya kupata matibabu.

Wataalamu wanaonya kuwa, iwapo ugonjwa huo utaenea sana Afrika basi bara hilo litashindwa kukabiliana na hali hiyo kutokana na mifumo dhaifu ya afya.