Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Wenyeviti wa mitaa 171 kutoka Kata 19, za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,mkoani Mwanza,wamepatiwa elimu ya utambuzi wa raia wa kigeni,ikiwa ni njia moja ya kukabiliana na wahamiaji haramu wanaoingia nchini kinyume na sheria.
Elimu hiyo imetolewa Aprili 12,2025 katika kikao cha kawaida cha kuwakumbusha Wenyeviti majukumu yao,iliofanyika makao makuu ya Halmashauri hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho,Mkaguzi wa Uhamiaji kutoka Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mwanza,Undule Haule,amesema,wanatarajia Wenyeviti hao watakuwa chachu ya kupeleka elimu hiyo kwa wananchi,ili waweze kuwasaidia katika mapambano dhidi ya wahamiaji haramu nchini.Kwani saula la ulinzi ni la watu wote ndani ya nchini.
Amesema maeneo korofi yanayoweza kuingiza wahamiaji haramu kwa Ilemela ni Sangabuye,Kayenze hasa kwenye Kisiwa cha Bezi,kwani ni rahisi watu kujificha,hivyo kwa sasa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ni nyenzo katika mapambano ya wahamiaji haramu.
Hata hivyo ametoa wito kwa Wenyeviti wa Mitaa,kuendelee kushirikiana na Uhamiaji kuhakikisha nchi inakuwa salama na tulivu bila uwepo wa wahamiaji haramu,ambapo amesema wakiwepo nchini wanaweza kuleta magonjwa,mitafaruku, migogoro,kupora ajira za wazawa pamoja na kuchangia mmomonyoko wa maadili.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Egidy Teulas,amesema,katika kikao hicho Wenyeviti wa mitaa yote ya Halmashauri hiyo,wamepatiwa elimu ya utambuzi kwa raia na kwa jinsi gani na kutumia njia gani ya kuwatambua raia na wasio raia wa Tanzania katika mitaa yao.
“Matarajio ni kuhakikisha tunapunguza wimbi la wahamiaji haramu wanaoingia katika Wilaya yetu na mitaa yetu,kwa sababu Wenyeviti hao wamefundishwa njia rasmi na za kisheria za kuweza kutambua wananchi ambao ni raia na wasio raia wa Tanzania,”amesema Teulas.
Kwa upande wake Ofisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU),Wilaya ya Ilemela,Rehema Abdallah,ametoa wito kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa,kutumia nafasi zao kuwatendea wananchi haki.
“Rushwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mamlaka uliopewa na umma kwa maslahi binafsi,hivyo timizeni wajibu wenu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu,ili kujiepusha na vitendo vya rushwa na kusababisha migogoro ambayo ina athari kwenye jamii,”amesema Rehema.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisiwa cha Bezi Kata ya Kayenze,James John,amesema kutokana na elimu alioipata, amejipanga kwenda kufanya mikutano ya hadhara ya kuzungumza na wananchi na wajumbe wake,kuona namna gani watapambana na wahamiaji haramu kwa kuwatambua,mazingira walipo na kazi wanazozifanya pamoja na kufahamu wameingiaje katika mtaa huo.
“Katika mtaa wa Bezi watu wengi wanaingia kupitia nafasi ya uvuvi kwaio tutashirikiana na na wamiliki wa mitumbwi kuwabaini wahamiaji haramu,kwani wao ndio wana waajiri.Natarajia kufanya kikao cha robo mwaka, na hiyo itakuwa moja ya ajenda,”amesema John.
Hata hivyo amesema,Serikali inapaswa kuongeza jitihada katika kukabiliana na uhamiaji haramu hasa maeneo ya Ziwa Victoria kwa kufanya opareshini kupitia Uhamiaji kwani wana utaalamu zaidi wa kubaini kwa urahisi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Pasiansi Magharibi Mariam Kisariya,amesema,mafunzo hayo yamemsaidia kujua jukumu alilo nalo kama kiongozi la kuhakikisha anakuwa mlinzi dhidi ya wahamiaji haramu, kwa kufahamu taariza za mwananchi mgeni anayekuwepo katika mtaa wake na kuchunguza kuwa ametokea wapi na utambulisho wake ni upi.
Pamoja na kuhakikisha wanazingatia sheria katika uongozi wao na kuepuka vitendo vya rushwa huku akiomba taasisi za Uhamiaji na TAKUKURU waendelee kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara ya mitaa.

More Stories
Hospitali ya Amana,kinara utoaji huduma za matibabu
Wadau waitwa kuchangia upauaji Maabara sekondari ya Mtiro
Coca-Cola yazindua Kampeni ya ‘Chupa la Machupa’