December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Teknolojia azindua Huduma ya NMB Mkononi Plus

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar

BENKI ya NMB imezindua huduma mpya ya NMB Mkononi Plus, ambayo Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Faustine Ndugulile, ameitaja kama muarobaini wa upotevu wa pesa na kichocheo cha kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za Bima na za kibenki kwa njia ya mtandao.

Uzinduzi NMB Mkononi Plus ‘Ya Wote,’ huduma inayotolewa kwa wateja na wasio wateja wa NMB, umefanyika Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Ndugulile na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa Usimamizi na Ukaguzi wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA), Neema Lutula.

Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Dk. Faustine Ndugulile (wa pili kushoto), Afisa Mkuu wa Biashara na wateja binafsi Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa tatu kulia), wakipiga makofi wakati wa uzinduzi wa huduma ya NMB Mkononi Plus uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkurugenzi wa Usimamizi na Ukaguzi wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA), Neema Lutula. Wapili kulia ni   Kaimu Afisa Mkuu Teknolojia na Mabadiliko ya Digitali wa NMB  Kwame Makundi na Mkuu wa kitengo cha Bima Martine Masawe (wa kwanza kulia) (Na Mpiga Picha Wetu).

Akizungumza kabla ya kuzindua huduma hiyo, Waziri Ndugulile amesema NMB Mkononi Plus ni huduma inayoakisi jitihada za benki hiyo katika kwenda na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita, ambayo imejikita katika kutokomeza foleni za kihuduma maofisini, sambamba na kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma za Bima na fedha kwa njia za mtandao.

“Ubunifu uendelee zaidi na NMB msiishie hapa, kwa sababu uzinduzi huu unaakisi utayari wenu katika kwenda na kasi ya Serikali, ambayo furaha yake ni kuona inaongeza idadibya watumiaji wa Bima na kutokomeza upotevu wa fedha, foleni za huduma maofisini, ambalo kwetu sisi sio jambo la sifa kamwe.

“NMB Mkononi Plus, ni muarobaini wa changamoto za kidijitali na tunaamini unaenda kuongeza kasi ya mafanikio yenu, ambayo ni kielelezo cha ubora wa huduma zenu uliowapa tuzo mbalimbali na pia unadhihirisha uimara wa uongozi wa benki hii chini ya watendaji wazalendo,” amesema Waziri Ndugulile.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Filbert Mponzi, alibainisha kuwa NMB Mkononi Plus ni huduma chanya kwa watumiaji wa huduma za simu za mkononi, bila kujali kama ni wateja ama sio wateja wa benki hiyo, ambayo imeanza kwa kutoa huduma tatu kubwa na muhimu.

Mponzi amezitaja huduma zilizo ndani ya NMB Mkononi Plus ni Bima Xpress (inayohusu huduma za bima), Dunduliza (inayohusisha Usajili Bima ya Afya) na Pamoja Akaunti (inayowezesha ufunguaji wa akaunti za vikundi), na kwamba huduma zaidi zitaongezwa katika mwamvuli huo kulingana na mahitaji ya wateja na wasio wateja.

“Leo hii kupitia NMB Mkononi Plus, tunathibitisha ubora na ubunifu tulionao, tunaosema kila uchao. Mkononi Plus ni ya wote, wateja na hata wasio wateja wetu, hii ni tofauti na ile huduma ya NMB Mkononi, ambayo ni maalum kwa wateja tu na sio zaidi.

“Wito kwa wateja ni kuwataka kuendelea kupata huduma bora na rafiki zitolewazo NMB, na wasio wateja wetu, tunawaomba waungane nasi kuhudumiwa na benki yetu, ambayo imeshinda tuzo kadhaa za kitaifa na kimataifa, huku tukijivunia kuwa wabunifu wa masuluhisho mbalimbali kupitia uwekezaji mkubwa wa kidijitali tuliofanya,” amesisitiza Mponzi.

Naye Mkurugenzi wa Usimamizi na Ukaguzi wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA), Neema Lutula, aliipongeza NMB kwa ubunifu uliozaa huduma hiyo, anayoamini itakuwa chachu ya kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za bima, ambao kwa sasa ni wachache.

“Sisi kama wasimamizi na bima nchini, tumefurahishwa na ujio a NMB Mkononi Plus, tukiamini unaenda kuchagiza watu wa kada zote kutumia huduma za bima na wito wetu kwa benki ni kuimarisha mahusiano mema na ushirikiano chanya na Kampuni za Bima nchini ili kurahisisha utoaji huduma kwa Watanzania,” amesema Lutula.