March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Afya Azindua Mkataba wa Huduma Bora kwa Wateja, Aagiza Utekelezaji wa haraka Nchini Kote


Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Dodoma

WAZIRI wa Afya,Jenista Mhagama, amezindua rasmi Mkataba wa Huduma Bora kwa Wateja utakaoongoza utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa na kuwaelekeza wananchi kuhusu haki na wajibu wao wanapopokea huduma za afyA ,Hafla ya uzinduzi huo imefanyika leo, Juni 25, 2025, jijini Dodoma.

Katika hotuba yake, Mhagama amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Seif Shekalage, kuhakikisha kuwa mkataba huo unatekelezwa kikamilifu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini, kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za kitaifa.

“Ndani ya muda mfupi, nataka kuona kila kituo cha afya nchini iwe ni Zahanati, Kituo cha Afya, Hospitali ya Wilaya, Rufaa za Mikoa na Kanda, pamoja na taasisi zote za afya kikiwa kimetekeleza mkataba huu. Hii ni kwa manufaa ya wananchi na watoa huduma wenyewe,” amesema Waziri Mhagama.

Amesisitiza kuwa lengo kuu la mkataba huo ni kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma kwa wakati, kwa weledi na kwa heshima, sambamba na kuwapa taarifa sahihi kabla ya matibabu ili kuongeza uwazi katika mchakato mzima wa huduma.

Aidha, Waziri huyo amesema utekelezaji wa mkataba huo ni sehemu ya kufikia dira ya Wizara ya Afya ya kuwa na jamii yenye afya bora na ustawi, itakayochangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa. Vilevile, mkataba huo utasaidia kupunguza malalamiko yasiyo na msingi na kuimarisha uwajibikaji kwa watoa huduma.

“Ni matarajio yangu kuwa kila mhusika atatimiza wajibu wake kupitia mkataba huu. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumepiga hatua kubwa kuelekea kwenye maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuibadilisha Sekta ya Afya kuwa bora na jumuishi zaidi,” ameongeza.

Waziri Mhagama pia amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia kwa kuwekeza katika rasilimali watu na vifaa tiba vya kisasa kama vile MRI, PET-Scan, na mashine za X-Ray ambazo zimeongeza uwezo wa utambuzi na matibabu nchini—vifaa ambavyo baadhi ya nchi bado hawana.

“Kazi kubwa iliyobaki ni kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi bila kikwazo cha fedha. Tayari tumeanzisha Bima ya Afya kwa Wote na kuhakikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuendeleza uwekezaji katika sekta ya afya,” alisema.

Kwa mujibu wa Waziri, huduma zilizojumuishwa katika mkataba huo ni pamoja na uhauri wa kitaalamu kuhusu uendeshaji wa shughuli za afya,huduma za chanjo,veti vya usajili wa kitaaluma,leseni na vibali mbalimbali, pamoja na upatikanaji wa taarifa muhimu za sekta ya afya.

“Kupitia mkataba huu, Wizara imejipanga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapohitaji huduma, anapata huduma bora, ya wakati na inayokidhi viwango vya kitaifa,” amesema Waziri Mhagama kwa msisitizo.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Shekalage, alieleza kuwa mkataba huo utasaidia kuimarisha mfumo wa utoaji huduma kwa kuongeza uwazi na uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa sekta ya afya