January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto Mh:Ummy Mwalimu,akionesha mfano wa kunawa katika moja ya matenki 1000 aliyoyakabidhi kwa mkuu wa mkoa wa Dar es salama kwa niaba ya mikoa mingine kwa ajili ya wananchi kunawa mikono kujikinga na maambukizi ya COVID 19

Waziri wa Afya akabidhi matenki 1000 ya kunawia mikono

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amekabidhi matenki 1000, sabuni na dawa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa niaba ya mikoa mingine kwa ajili ya wananchi kunawa mikono kujikinga na maambukizi ya Covid-19.

Waziri Ummy Mwalimu amesema katika Mkoa wa Dar es Salaam, wamepatiwa matenki 350 na kwamba mikoa mingine watapatiwa matenki 26 na kwamba lengo ni kuwawezesha wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya maambukizi ya Covid-19.

“Kwanini Dar es Salaam imepatiwa vifaa vingi, ni kwa sababu wenyewe wana maeneo mengi ya wazi na lakini tukiangalia Dar es Salaam kuna wagonjwa wengi walioambukizwa virusi vya Covid-19,” amesema Ummy Mwalimu.

Akizungumzia mwenendo wa wagonjwa wa Covid-19, Ummy Mwalimu amesema watu wawili wamepona na kwamba mgonjwa mmoja wa Dar es Salaam na Arusha wamepona na wameruhusiwa kurejea nyumbani.

Waziri Ummy Mwalimu amefafanua kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na Arusha hakuna wagonjwa wa Corona hivyo wagonjwa waliobaki kwenye vituo maalumu vya kutoa tiba wamebaki 18 na kwamba kesi za wagonjwa walioambukizwa COVID 19 hadi sasa ni 24.

Amesisitiza kwamba wasafiri wanaotoka katika nchi zilizoathirika wataendelea kukaa karantini katika hosteli za Magufuli jijini Dar es Salaam na amebainisha kuwa Changamoto wamezipokea na kwamba zinafanyiwa kazi.

‘Serikali haina mchezo na suala la karantini, hakuna mbadala wa mtu kutokaa katika hosteli za Magufuli kwani kipaumbele Cha Serikali ni kuhakikisha maambukizi yaliopo ndani hayasambai zaidi,’amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Amesema lengo la wasafiri kuwekwa karantini katika hosteli hizo ni kuzuia maambukizi mapya kutoka nje ya nchi na amewataka wakuu wa mikoa kuwa makini katika kusimamia suala la karantini ili Kuzuia wenye maambukizi wasiingie nchini.

Pia, Waziri amewataka wagonjwa waliopona kujitunza kwani takwimu kutoka China zinaonyesha kwamba katika kila watu 100 waliopona COVID 19, 14 wanaweza kuambukizwa Tena ugonjwa huo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kuwa wasafiri wote wanaopelekwa katika hosteli za Magufuli hawatatoka nje ya hosteli hizo kwani lengo ni kuwaokoa wananchi wasiambukizwe virusi vya Corona.

Makonda amesema kuwa matenki hayo yatawekwa katika vituo vya daladala, sokoni na maeneo mengine ya wazi na amewahimiza wananchi kunawa mikono mara kwa mara na maji yanayotiririka ili Kuzuia maambukizi.

“Napenda kuwashukuru viongozi wa dini kwa kufungua na kuombea nchi ili kusiwe na maambukizi mapya kwa Watanzania,” amesema.

Msaada wa vifaa vimetolewa na Subhash Patel na vina thamani ya Shilingi milioni 300 wakati dawa, sabuni na barakoa ambazo zina thamani ya Shilingi milioni 10 zimetolewa na Hospitali ya Aga Khan.