Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Wananchi wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida kuzitunza barabara zilizojengwa na Serikali ili ziweze kudumu muda mrefu.
Mhe. Ummy ametoa ombi hilo wakati akizungumza na wananchi hao wakati akikagua barabara ya Singa- Kinampundu-Ilunda iliyojengwa kwa kiwango cha changarawe katika ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Jambo lililokubwa niwatake wananchi mzitunze hizi barabara kwa sababu Serikali inazitengeneza lakini kunawananchi wanapitisha majembe ya kukokotwa na ng’ombe na vitu vingine vinavyoharibu barabara kwa hiyo niwatake ulinzi wa barabara uwe ni jukumu letu sote kwa sababu fedha zilizotumika kuzitengeneza ni nyingi hivyo tunatamank ziendelee kuwa na ubora na zisaidie kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi” alisema Waziri Ummy.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Belinth Mahenge amesema hivi karibu wameshasaini Mikataba 16 yenye thamani ya sh. Bil 12.5
kwa ajili ya ujenzi wa barabara mbalimbali za Mkoa wa Singida.
Bajeti ya barabara kwa Mkoa wa Singida imepanda kutoka sh. Bil 6.1 kwa mwaka 2020/21 mpaka sh. Bil. 22.4 hivyo barabara nyingi za mkoa huo zitaimarika kutoka na ongezeko la Bajeti hiyo.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji wa Wilaya ya Mkalama, Edward Masola alisema matengenezo ya barabara hiyo yatagharimu kiasi cha Sh.milioni 91,201,000.
Alisema barabara hiyo ambayo inaunganisha Kata za Ilunda na Kinampundu itakapokamilika itarahisisha usafiri kwa wananchi kufikia huduma za elimu, afya na masoko.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja