November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ulega aridhishwa na utekelezwaji wa miradi ya maendeleo Iringa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema amefurahishwa na Uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa namna wanavyosimamia utekeleza wa miradi ya maendeleo hususan kwenye sekta ya elimu.

Waziri Ulega amesema hayo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya shule za sekondari zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini Oktoba 2, 2024.

“Leo nimekuja kuona kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kulijenga taifa hapa Iringa, nimekagua miradi yote na nimeridhika fedha zimetumika vizuri sana, hongereni viongozi kwa kusimamia vyema fedha hizo”, amesema

Waziri Ulega alimshukuru Rais Samia kwa kujenga miundombinu ya kisasa ya shule mkoani Iringa akisema kuwa hatua hiyo sio tu inaimarisha sekta ya elimu bali imekwenda kutatua changamoto kubwa za msongamano wa wanafunzi madarasani lakini pia kuwapunguzia watoto kutembea umbali mrefu kwenda shuleni na kurudi nyumbani.

“Miaka michache nyuma viongozi wa halmashauri za wilaya walikuwa wanagombea miradi, lakini katika kipindi hiki cha miaka takriban 4 ya Rais Samia jambo hilo ni historia, amepeleka pesa nyingi za miradi mbalimbali katika halmashauri ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya shule na sasa inatekelezwa kila mahala”, amefafanua

Aidha, pamoja na kuupongeza uongozi huo wa mkoa, Waziri Ulega amewahimiza pia kuhakikisha wanatangaza vyema kazi hiyo kubwa inayofanywa na Rais Samia ili wananchi waweze kujua, kutambua na kuitunza miradi hiyo ya maendeleo inayotekelezwa na serikali yao.

Katika ziara yake hiyo, Waziri Ulega amekagua bweni la wanafunzi lililojengwa katika shule ya Sekondari ya Ifunda, amekagua ujenzi wa Madarasa 7 na matundu ya vyoo 16 katika shule ya Sekondari Kiwere, amekagua ujenzi wa Madarasa 6 na matundu ya vyoo 8 katika shule ya Sekondari Pawaga na amekagua na kuzindua shule mpya ya Sekondari Mboliboli.