Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry Slaa amesema kuwa anwani ya makazi ni muunganiko wa taarifa na miundombinu ambayo kwa pamoja inatambulisha anuani halisi ya kitu au mtu alipo ili kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma.
Slaa amesema hayo jijini hapa leo,Februari 6,2025 wakati akifungua maadhimisho ya kwanza ya Wiki ya Anwani za Makazi nchini ambayo kwa mwaka huu Kitaifa yanafanyika Jijini Dodoma yakiwa na kauli mbiu inayosema” TAMBUA NA TUMIA ANWANI ZA MAKAZI KURAHISISHA UTOAJI NA UPOKEAJI WA HUDUMA”
Amesema kuwa kwa kutambua hilo Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na wadau wengine hususan Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaratibu utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi nchini.
“Hatua hii ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003, makubaliano ya Kikanda na Kimataifa kupitia Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na Umoja wa Posta Duniani (UPU),na Ibara ya 61(m) ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila nyumba, jengo, kiwanja, huduma, ofisi ama eneo la biashara linatambulika kwa Anwani ya Makazi,anwani ya Makazi inaundwa na Namba ya Anwani maarufu kama namba ya nyumba,Jina la Barabara au Mtaa na Postikodi.
“Postikodi ama nchi zingine zinaita Zipcode ni utaalamu wa kugawa maeneo ili kurahisisha utambuzi. Kwa hapa Tanzania mgawanyo huu umefanyika katika ngazi ya kata ambapo kila Kata ina Postikodi yake yenye tarakimu tano”amesema Slaa.
Amesema kuwa anwani za Makazi inarahisisha utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya Kiuchumi na kijamii hasa katika zama hizi ambazo Mapinduzi ya 4,5 na 6 ya viwanda yanategemea matumizi ya TEHAMA. Na matumizi ya TEHAMA yanalazimu kuwa na mifumo ya utambuzi ndiyo sababu ya Serikali kuanzia mfumo huu.
“Itakumbukwa kwamba utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ulianza mwaka 2010 na kwa mujibu wa Mpango wa utekelezaji ulitakiwa ukamilike mwaka 2015 hata hivyo, utekelezaji wake ulikuwa wa kasi ndogo ukilinganisha na matarijio, hali iliyosababisha kuanzishwa kwa Operesheni maalumu iliyojulikana kama Operesheni Anwani za Makazi ambayo ilizinduliwa na Rais, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 08 Februari, 2022. Operesheni hiyo ilifanyika nchi nzima na kusimamiwa na wakuu wa mikoa Tanzania Bara na Zanzibar,”amesema Waziri Slaa.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za mikoa na Serikali za mitaa(TAMISEMI) Dkt.Festo Dugange akizungumza Kwa niaba ya Waziri ya Waziri wa Wizara hiyo,Mohamed Ncheregwa amesema kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi ni nyenzo ya utambuzi ambayo inatambulisha wakazi na makazi na uwepo wa mfumo huo kwa upande wa OR-TAMISEMI ni nyenzo muhimu zaidi kwani kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Serikali za Mitaa, jukumu la kutoa majina ya mitaa lipo OR-TAMISEMI, hivyo utekelezaji wa mfumo huu unarahisisha utekelezaji wa jukumu la kutoa majina ya mitaa kama ambavyo kauli mbiu ya maadhimisho haya inavyosema.
Aidha amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI ni mdau mkuu katika utekelezaji hususan kupitia kwa Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa ambao wana wajibu wa kuwezesha uwekaji wa miundombinu,kuhuisha taarifa, na kukusanya taarifa mpya.
“Lakini pia TAMISEMI ni mnufaika mkubwa katika matumizi ya Mfumo,hii ni kwa kuzingatia kwamba Mfumo unawezesha utambuzi hivyo hurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma.
“TAMISEMI ndiyo yenye wananchi na ndiyo mtoa huduma mkuu kwa wananchi, hivyo TAMISEMI inauhitaji sana Mfumo huu na kwa sasa tulifanya majaribio ya kutoa barua kwa njia ya kidijitali ambapo jambo hilo limeonyesha kuwa la mafanikio”amesema.
More Stories
Kampuni ya ununuzi wa tumbaku yarejesha faida kwa jamii
Rais Samia awaonya Majaji na Mahakimu
Mwabukusi akerwa na wanaodai amelamba asali