November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Simbachawene akabidhi mradi ujenzi wa kituo cha usimamizi wa maafa Dodoma

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amekabidhi rasmi mradi wa ujenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Maafa kilichopo eneo la Nzuguni “B” Jijini Dodoma kwa mkandarasi Lwanda Limited kutoka Morogoro.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika tarehe 14 Mei, 2022 na kuhudhuriwa na viongozi wa ofisi yake pamoja mshauri elekezi na mkandarasi amewataka kukamilisha mradi huo kwa wakati kwa kuzingatia umuhimu wa kituo hicho katika kuratibu shughuli za maafa nchini.

Aliongezea kuwa, tayari fedha zimeshatolewa kiasi cha shilingi bilioni 2.442 ambazo zitatumika kuhakikisha ujenzi unaanza haraka bila kukwama.

“Kipekee nimpongeze Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha kuhakikisha ujenzi unaanza ili kuendelea kuratibu masuala ya maafa kwa ufanishi mkubwa hivyo ipo haja ya kuifanya kazi hii kwa weledi na kuikamilisha kwa wakati,”

Uwepo wa kituo utasaidia kuongeza hali ya usalama katika anga, nchi kavu na kwenye maji kwa kuzingatia jitihada za serikali katika kuhakikisha usalama wa wananchi ili kuendelea kushiriki katika shughuli za kimaendeleo kwa utulivu.

Akitoa taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mumanga alisema mradi umetengewa eneo la  ukubwa wa ekari 106 hivyo kituo kinatarajiwa kuwa kikubwa chenye kukidhi mahitaji yaliyopo nchini ili kutoa huduma kwa viwango vinavyotakiwa.

“Muda wa utekelezaji wa mradi ni miezi 12 baada ya makabidhiano ya eneo la kazi na kazi zitaanza rasmi tarehe 30 Mei, 2022 na tunatarajia mkandarasi aukabidhi mradi huu tarehe 29 Mei, 2023,”alieleza Meja Jenerali Mumanga

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene akikabidhi nyaraka kwa mkandarasi kutoka LADWA limited wakati wa hafla ya kukabidhi mradi wa Kituo cha Usimamizi wa Maafa nchini kitakachojengwa katika eneo la Nzuguni ‘B’ Jijini Dodoma.Halfa hiyo ilifanyika tarehe 14 Mei, 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene akiangalia michoro ya ramani inayoonesha muonekano wa mradi wa Kituo cha Usimamizi wa Maafa utakavyokuwa mara baada uya ujenzi, anayetoa maelezo hayo ni Meneja wa mradi huo Dkt. Godwin Maro.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene akikata utepe ikiwa ni ishara ya kukabidhi rasmi mradi wa ujenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Maafa kwa mkandarasi wa LADWA limited tarehe 14 Mei, 2022 Nzuguni ‘B’ Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mumanga akitoa taarifa kuhusu mradi wa ujenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Maafa wakati wa hafla ya makabidhiano ya mradi huo kwa mkandarasi LADWA limited
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mumanga mara baada ya kuwasili katika hafla ya kukabidhi mradi huo.

Baadhi ya washiriki wa hafla ya makabidhiano ya mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Maafa wakifuatilia hafla hiyo
Baadhi ya washiriki wa hafla ya makabidhiano ya mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Maafa wakifuatilia hafla hiyo