Na Prona Mumwi,Timesmajira
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, ameweka wazi mikakati yake ya kuboresha sekta ya habari kupitia ushirikiano wa karibu na wanahabari.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wadau wa sekta ya habari kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025, Waziri Silaa amesema amejipanga kuhakikisha sekta ya habari inaimarika kwa kufanya marekebisho ya sera na sheria ili kuendana na mahitaji ya kisasa.
Waziri ameeleza kuwa sekta ya habari ni mhimili muhimu katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kiusalama, huku pia ikiwa nguzo ya utawala bora. Amesema serikali inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kusimamia uwazi na uwajibikaji, na kwa sasa kuna vyombo 1,023 vya habari ambavyo vinatoa mchango mkubwa kwa taifa.

Akiwa na dhamira ya kuboresha sekta hiyo, Waziri Silaa amesema atatembelea wadau wote wa habari, akianza na makundi, na hatimaye vyombo vya habari binafsi, ili kujadiliana na kubadilishana mawazo. Pia ameongeza kuwa marekebisho yaliyofanywa kwenye sheria na kanuni yamewaondolea wanahabari adhabu za kijinai kwa makosa ya kashfa na yameimarisha uhuru wao wa maoni, upatikanaji wa habari, na uhariri wa maudhui bila hofu.

Waziri amepongeza wanahabari kwa kufanikisha mawasiliano kuhusu miradi ya maendeleo ya serikali na kuwahamasisha kuendelea kufuata sheria, kanuni, na maadili ya kazi hasa katika kipindi cha kampeni na uchaguzi. Amesisitiza kuwa historia ya tasnia ya habari nchini ni msingi wa umoja wa kitaifa, akirejelea mchango wa vyombo vya habari katika harakati za uhuru na ujenzi wa taifa ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Kwa ujumla, Waziri Silaa amesisitiza dhamira yake ya kushirikiana na wanahabari kuhakikisha sekta ya habari inatoa mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya Tanzania.
More Stories
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Baraza la Taifa la Ujenzi waingia makubaliano ya mashirikiano sekta ya ujenzi
Nderiananga aongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu ujerumani
Taarifa za maendeleo ziwafikie wananchi kwa usahihi