Na Penina Malundo,Timesmajira
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu amesema anaendelea kukutana na wadau mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha mahusiano na kukusanya maoni yatakayosaidia kuandaa nyaraka za kuimarisha ushirikiano wa kitaifa.
Akizungumza Februari 13, 2026 mkoani Dodoma alipotembelea Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Sangu amesema baraza hilo ni mdau muhimu katika kutekeleza majukumu ya wizara hiyo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefungua milango kwa wadau wote wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dini na vyama vya siasa ili kushirikiana katika kujenga taifa lenye mshikamano.

“Tumekutana kujadili namna ya kuimarisha mahusiano na kuendeleza ushirikiano. Msingi wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa,” amesema Sangu.
Amesema NaCoNGO imeahidi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kulinda amani na kusimamia maadili kupitia vyombo vyao vya ndani ili kuhakikisha mashirika wanachama yanafuata miiko na taratibu walizojiwekea.
Sangu amebainisha kuwa zaidi ya mashirika 8,000 yaliyo hai nchini yana mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NaCoNGO, Jasper Makala amemshukuru Waziri Sangu kwa kutembelea ofisi za baraza hilo, akisema ziara hiyo imeimarisha mazungumzo na ushirikiano kati ya Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Amesema kuanzishwa kwa Idara ya Mahusiano chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni hatua muhimu itakayosaidia kuboresha zaidi mahusiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali nchini.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina