Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amekemea vikali mmomonyoko wa maadili shuleni na kuwataka walimu na wazazi kushirikiana ili kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na malezi bora.
Akizungumza katika mahafali ya shule za kiislamu za Ilala Mkoa wa Dar es salaam leo Novemba 06, 2022 Waziri Prof. Mkenda amesema kuwa ni lazima kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa malezi bora kutoka kwa wazazi pindi wanapokuwa nyumbani na walimu wakati wakiwa shule ili kuepukana na mmomonyoko wa maadili
Aidha, Prof. Mkenda amesema lugha ya kiarabu hufundishwa na dini ya kiislamu na ni lugha ya kwanza kutoka nje ya taifa letu, hatuwezi kufundisha kufaransa, kiingereza, kichina halafu kiarabu tukaacha kufundisha jambo ambalo litasaidia kwenye imani yao.
“Lugha ya kiarabu ni lugha nadhani ya pili au ya kwanza kwa kuzungumzwa katika bara la Afrika na ni lugha namba mbili Duniani katika shirika la umoja wa Mataifa, hivyo kweli itatusaidia sisi kuandaa watu ambao watatumia kiswahili kama wakalimani kwa sababu lazima mkalimani ujue lugha kadhaa” amesema Mkenda
Waziri Mkenda amesisitiza kuwa ombi la masomo ya dini kupewa msukumo sawa na masomo mengine shuleni amewataka viongozi hao kuwa na subira kwanza, hatua hiyo imekuja baada ya maombi ya viongozi wa dini juu ya masomo hayo kutojumuishwa kwenye vigezo vya kujiunga na vyuo.
“Huu mjadala wa masomo ya dini kufundishwa shuleni tuliache kwanza, kwamba mtu anapochukua somo la dini liwe katika masomo yanayohesabika kuna sababu kadhaa lazima tuzizingatie hivyo siwezi kulizungumzia kwa sasa”
“Kuhusu vibali vya kufungua shule kwa kweli kwa mjini changamoto kubwa ni ardhi, tutaanza kuliangalia upya kwamba si lazima eneo liwe kubwa sana pengine lazima uende juu, kuna shule moja katika mkoa fulani ilikuwa inatakiwa kufungwa lakini baada ya kujionea nilitoa maelekezo maana walikuwa tayari wameshaanza na haikuwa busara kuwaambia wasitishe masomo” amesema Mkenda
Kwa yeyote anayetaka kuanzisha shule hapa mjini kwa masharti yetu inaweza kuwa changamoto, lazima masharti yabadilike kwa ujumla wake, hivyo tuendelee kushirikiana na serikali hakuna litakaloshindikana.
Kwa upande wake Shekh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam amewataka watanzania na wadau wa elimu nchini kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu nchini
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua