Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa utendaji mahiri ambao umesaidia kuleta mageuzi kwenye sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji nchini.
Akipokea jana taarifa ya utendaji wa kimkakati wa TADB iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Japhet Justine ofisini mwake jijini hapa, Waziri Nchamba amesema utendaji mahiri wa TADB unasaidia kuyapa maana machoni mwa Watanzania maono ya Rais Samia Hassan juu kilimo.
“Niwapongeza kwa kutekeleza haya yote ambayo mmeyawasilisha hapa. Ni dhahiri kuwa mmefanikisha mengi na mipango yenu ni yenye mkakati wa kuwezesha maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yaeleweke kwa Watanzania juu ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo,”amesema Dkt. Nchemba.
Naye Katibu Mkuu wa Hazina, Emmanuel Tutuba, ameeleza kuridhishwa na ripoti ya benki hiyo na kusema anaona jitihada ya dhahiri ya benki hiyo katika kuendeleza na kutimiza wajibu uliowekwa na serikali ili utimizwe na taasisi hiyo.
Akitoa taarifa hiyo, Justine amemueleza waziri kuwa tangu kuanzishwa kwa benki hiyo zaidi ya wakulima 1,800,000 wamefikiwa.
“Pamoja na kuwafikia wakulima hawa, lengo la Serikali la kuanzisha benki hii ni pamoja na kuchachusha upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wadau katika sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo,” amesema .
Justine, na kuongeza: “Kipekee Mhe. Waziri tumeweza kushawishi kushuka kwa kiwango cha riba zilizokuwa zikitolewa na benki na taasisi za kibiashara za fedha kutoka asilimia 24 hadi kuwa kati ya asilimia 17 na 14.”
“Ni nia yetu sasa kuendelea kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi na kasi inayoendana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha utoshelevu wa chakula ndani ya nchi, kuongeza uzalishaji, na upatikanaji wa malighafi za viwanda,” ameeleza Justine.
Ameieleza hafla hiyo kwamba malengo lingine ya benki hiyo ni kufungamanisha wakulima wanaozalisha mazao na masoko, na kuboresha miundombinu ya kilimo kwa kuhakikisha upatikanaji wa zana bora za kilimo na uvuvi, upatikanaji wa pembejeo na viwatilifu kwa wakulima. Kadhalika ni kuwezesha ujengaji wa maghala na viwanda vidogo vidogo vya kuchakata mazao ili kupunguza upotevu na uharibifu wa mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji. alisisitiza Justine.
Katika ujumbe wa TADB alikuwemo Mkurugenzi wa Fedha, Derick Lugemala, Kaimu Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara, Bi. Afia Sigge, na Meneja wa Kanda ya Kati, Yodas Mwanakatwe.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi