Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dar
WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Geoffrey Mwambe ameahidi kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) sambamba na kuongeza ufanisi katika kuimarisha mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao chake na menejimenti na wafanyakazi wa TNBC juzi, Mwambe amesema Baraza kama taasisi ni kiungo muhimu kati ya sekta za umma na binafsi na hivyo kuimarika kwake kutaleta matokeo chanya ikiwemo kukua kwa biashara na kuongezeka kwa uwekezaji.
“Kuongezeka kwa ufanisi wa Baraza kutaliongezea na kutoa mchango stahiki wa kuziunganisha sekta za umma na binafsi kufanya majadiliano ya namna bora ya kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza mapato ya Serikali,” alisema Waziri Mwambe.
Waziri Mwambe aliyefanya ziara yake ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo hivi karibuni, amesema ili taifa lisonge mbele kiuchumi lazima kuwe na sekta binafsi madhubuti na ambayo itakuwa jumuishi.
Amesema licha ya uchanga wa wizara, yeye na timu yake watahakikisha wanashirikiana na wadau wote katika sekta za uwekezaji, biashara na taasisi zote zilizopo kwenye wizara hiyo kuweka mikakati ya namna bora ya kuvutia zaidi uwekezaji na biashara.
“Mimi na timu yangu tumekuja kuona namna TNBC wanavyofanya kazi, kusikiliza changamoto zao pamoja na kupokea mawazo. Tunakusudia kuzileta pamoja sekta ya umma na binafsi kwa kuondoa changamoto na kuongeza ufanisi,” amesema.
Waziri Mwambe mbali ya kuipongeza TNBC, alisema Baraza lina nafasi kubwa ya kuhakikisha sekta za umma na binafsi zinafanya kazi kwa karibu zaidi na kuongeza wigo wa uwekezaji na kuchocheo ongezeko la ajira kwa vijana na pia kuongeza mapato ya serikali.
TNBC kama taasisi inayounganisha sekta za umma na binafsi, uendeshwaji wa shughuli zake inatakiwa zichangiwe kwa ubia wa pande zote mbili. Hata hivyo, michango bado inatolewa na serikali tu.
Waziri Mwambe ameahidi pia kufanya mazungumzo na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) hivi karibuni kuona namna bora ya ushiriki wake katika TNBC ili kupiga hatua mbele ya maendeleo ya Taifa.
Aidha, Waziri alizitaka taasisi zote za umma kuachana urasimu, rushwa na kuwa rafiki kwa wawekezaji ili kufanikisha kufikiwa kwa malengo ya ukuaji wa uchumi unaokadiriwa kukua kwa asilimia nane kwa mwaka.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga amemhakikshia Waziri na timu yake kuwa Baraza litatoa ushirikiano mkubwa ikiwemo kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuwavutia uwekezaji.
“Tumekuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kibajeti, upungufu wa watumishi ili kufanikisha majukumu yetu. Ni matumaini ya baraza kuwa uteuzi utasaidia sana kuleta mabadiliko katika sekta za biashara na uwekezaji hapa nchini,” amesema Dkt. Wanga.
Amesema Baraza kwa mwaka 2021/22 imejipanga kuendelea kufanya ufuatiliaji na tathmini kuhusu utekelezaji wa maboresho ya mazingira ya biashara, kufanya tafiti za kina na kuishauri serikali.
More Stories
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto
Walimu S/ Sekondari Ilala wafundwa juu ya maadili ya wanafunzi
Dkt. Samia afungua skuli ya sekondari Misufini, Bumbwini