Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametoa mwezi mmoja kwa maofisa wa Serikali kuwasaka na kuwakamata watu wote wanaojihusisha na uingizaji wa mazao ya mifugo nchini ikiwemo maziwa na kuwachukuliwa hatua kali za kisheria ili kulinda uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika nchini kwa sasa.
Pia Wizara imepokea maelekezo kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kupitia Mwenyekiti wake, Mahmoud Mgimwa ya kuitaka Serikali kupiga marufuku matumizi ya maziwa ya unga kama NIDO, Lactogen kutoka nje ya nchi katika Ofisi za Serikali.
Waziri Mpina amesema suala hilo litasimamiwa kikamilifu na Wizara yake ili kuhamasisha viwanda vya ndani kuongeza uzalishaji na kupunguza uagizaji wa maziwa kutoka nje ya nchi.
Hivyo katika kipindi hicho cha mwezi mmoja kuanzia sasa amemuagiza Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo (DVS), Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko (DPM), Bodi ya Maziwa (TDB) na Bodi ya Nyama (TMB) kuongeza udhibiti kupitia Operesheni Nzagamba ili kuzuia kwa namna yoyote uingizaji wa mazao ya mifugo nchini bila ya kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu.
Akizungumza wakati wa Kilele cha Wiki ya Maziwa yaliyofanyika Kitaifa jijini Dodoma kwa njia ya Kielektroniki, Waziri Mpina alisema kamwe Tanzania haiwezi tena kukubali kukubali kugeuzwa soko la bidhaa zinazoingizwa kiholela kutoka nje ya nchi huku akitaka hatua za kuimarisha uwekezaji nchini ziendelee kuchukuliwa.
Pia amegiza wanunuzi wote wa maziwa hasa wasindikaji kuzingatia mwongozo uliotolewa na Wizara wa kununua maziwa ghafi kwa bei isiyopungua sh. 800 kwa lita ya maziwa ili kufidia gharama za uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kuchochea uzalishaji zaidi kwa wafugaji;
Mbali na hilo pia ameagiza kuzingatiwa bei elekezi ya shilingi 10,000 kwa uhimilishaji kwa ng’ombe bila vichochezi kama ilivyowekwa katika Kanuni ya Artificial Breeding Regulation 2020 kwani Kanuni hizi zimetungwa ili kuweka usimamizi thabiti wa uhimilishaji nchini na kuweka bei elekezi ambayo inatoa unafuu zaidi kwa wafugaji badala ya kiwango cha zamani cha zaidi ya shilingi 25,000 kwa ng’ombe.
Hivyo Waziri Mpina ameziagiza Sekretarieti zote za Mikoa, Halmashauri zote za Wilaya kuzingatia na kusimamia kikamilifu matumizi ya Bei elekezi kwa chanjo 13 za magonjwa ya kimkakati katika kutoa huduma kwani tayari wizara imeshatangaza Bei elekezi ya chanjo za kimkakati na kusambazwa nchi nzima, hivyo mtu yoyote atakayekiuka achukuliwe hatua kali za kisheria.
Mbali na hilo pia Waziri Mpina amewataka Wafugaji kote nchini kuongeza uzalishaji, kutumia vizuri fursa zinazotolewa na Serikali na kuendelea kuwafuga ng’ombe wa maziwa kwa tija.
Pia Wasindikaji na Wamiliki wa Viwanda wametakiwa kusindika maziwa kulingana na uwezo wa viwanda (Installed capacity) kuliko ilivyo sasa ambapo wanasindika asilimia 23.52 tu ya uwezo wao jambo linalosababisha maziwa mengi kumwagwa kwa kukosa soko na kusababisha maziwa mengi kutokusindikwa jambo ambalo hupelekea kuendelea kutegemea kuagiza maziwa kutoka nje ya nchi;
“Ninaagiza katika kipindi cha miaka miwili ijayo nchi yetu isiagize tena maziwa kutoka nje ya nchi, wadau wote wanaagizwa kuweka mikakati madhubuti kufikia malengo hayo. Nchi yetu ina ardhi yenye rutuba, ina malisho bora na mifugo mingi, hatuwezi kuendelea kuagiza maziwa kutoka nje ya nchi. Tena wakati mwingine tunaagiza maziwa kutoka nchi ambazo hazina hata mifugo, Suala hili halivumiliki tena”amesema Waziri Mpina
Waziri Mpina alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kukusanya maoni kutoka kwa wadau, kufanya utafiti na tathmini za kina kuondosha kero na changamoto zote zinazoikabili tasnia ya maziwa.
“Tulishakataa nchi yetu kugeuzwa kuwa dampo la bidhaa kutoka nje ya nchi, Tulishakataa kukatishwa tamaa katika dhamira tuliyoiweka ya kuwatumikia watanzania na tulishakataa kurudi nyuma. Nitoe rai kwa watanzania wote kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano katika jitihada inazofanya”amesisitiza Waziri Mpina
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji aliitaka Serikali kupiga marufuku matumuzi ya maziwa ya unga ya Nido na Lactogen ili kuhamasisha uwekezaji wa ndani kwani maziwa mengi yamekuwa yakimwagwa kwa kukosa soko.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini