January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu Majaliwa mgeni rasmi kongamano la TAWECE

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la Wahandisi wanawake (TAWECE) la mwaka huu litakalofanyika julai 29, 2022 katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es salaam.

Hivyo, kutakuwa na tuzo za Mama mhandisi Award ambazo mwaka huu zitatolewa kwa mara ya pili tangu ziazishwe mwaka 2021, kwa kutambua mchango wa wanawake mwaka huu kutakuwa na tuzo ya Mhandisi mwanamke wa mwaka, mhandisi mwanamke kiongozi wa mwaka na mhandisi mwanamke mbunifu wa mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari leo julai 20, 2022 jijini Dar es salaam katibu wa Taasisi ya Wahandisi – kitengo cha wanawake Ester Christopher amesema taasisi zote zenye wahandisi wanawake na mafundi ziwaruhusu na kuwalipia ili waweze kuhudhuria kongamano hilo lenye dhumuni kubwa la kuhamasisha wanawake kujiunga na fani ya uhandisi.

”Dhumuni hili hutekelezwa kwa kutembea shule za sekondari na kuhamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi ili kufikia taaluma ya uhandisi, itawasaidia kuondoa dhana potofu kwamba masomo ya sayansi ni kwa ajili ya wanaume tu” amesema

Aidha, faida za kuhudhuria kongamano hilo ni pamoja na kuwajengea uwezo wahandisi wanawake kutoka kwa wawasilishaji wa mada wabobezi ili kupata mawazo ya kibiashara na kuboresha au kuibua suluhu mpya katika miradi ya kiubunifu inayowasilishwa, kukutana na kujenga mtandao (networking) kupongezana na kutambuana kwa michango mikubwa ambayo wahandisi wanawake wamekuwa wakifanya katika jamii.

Kongamano hilo hutambulika kwa jina la TAWECE (Tanzania Women Engineers Convention Exthibitions) hivyo wafadhili watakaoweza kuwalipia gharama za ushiriki wa wanafunzi na wahandisi wahitimu wajitokeze kwa wingi ili tupate ushiriki wao wa kutosha na kwa taasisi ambazo hazijajiunga zijiunge kwa kupitia tovuti ya www.ietwc.or.tz.