January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu Majaliwa awapa rungu TANAPA kuendelea kusimamia vivutio vya utalii

Na Esther Macha, Timesmajira, Online,Mbeya

WAZIRI Mkuu wa Kassim Majaliwa amesema ipo haja kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuendelea kujipanga na namna ya kusimamia maeneo yote yenye vivutio vya utalii nchini.

Majaliwa amesema hayo alipotembelea banda la TANAPA lilipo ndani ya Q banda la Wizara ya Maliasili na Utalii wanaoshiriki maonesho ya kimataifa ya wakulima Nane Nane yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.

“Matumaini yetu mnatupeleka kwenye mafanikio makubwa muhimu endeeleni kujipanga vizuri namna ya kusimamia maeneo yote yenye vivutio kuanzia Songwe kwenye kivutio cha kimondo na maeneo mengine yote yenye wanyama ,mito na vitu vingine ambavyo mnasimamia hata haya maeneo ya kumbukizi ya Chief Mkwawa nayo bado ni maeneo yenu haya ni maeneo muhimu “amesema Waziri Mkuu.

Hata hivyo Waziri Mkuu amesema ipo haja kwa TANAPA kuendelea kuvitumia vyombo vya habari katika kutangaza shughuli za TANAPA ili kueleza shughuli za shirika na vivutio.

“Tunaona eneo la Mikumi wanyama wamepungua kidogo ukilinganisha na zamani mmepeleka zaidi Serengeti tengeni usawa katika maeneo haya watalii wasirundikane sehemu moja wapite maeneo yote,”.

Aidha amesema kuwa hakuna shida ya usafiri serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga miundombinu mizuri kwenye maeneo yote ya vivutio vya utalii ambapo utalii ukishamili sekta ya kilimo na mifugo itapata tija nyama zitapatikana na samaki zitaliwa hivyo uwepo wao kwenye maonesho hayo ni sehemu sahihi na wanaongeza dhamani kubwa.

“Hii programu ya Royar Tour ya Rais Dkt.Samia imeleta mafanikio makubwa sana kwa hiyo na nyinyi lazima muende kwa spidi zaidi kuliko Royar tour, endeeleni kuhifadhi maeneo yenu na simamieni vivutio vyetu,juzi nilikuwa nazungumza na Balozi wa Urusi wanataka kuleta ndege wanakamilisha makubaliano ya nchi na nchi,”amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema wakishakubaliana usalama wa ndege na watumishi wao wataanza kuleta ndege zao na historia inaonesha kuwa miaka 10 iliyopita wakati ndege za Urusi kipindi zinakuja wamewahi kupata watalii zaidi ya 72,000 Kwa mwaka kutoka Urusi tu .

” Ndo maana tunataka kurudisha idadi ile sasa chukua ulionao sasa na ndege zikishaanza na idadi hiyo ikiongezeka ndo sababu nasema lazima muende mbali zaidi,tangazeni utalii kwa bidii kubwa na hongereni kwa kazi nzuri “amesema

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi – TANAPA, Theodora Aloyce akimkaribisha Waziri Mkuu amesema shughuli za uhifadhi wa vyanzo vya maji vinavyopatikana katika hifadhi za taifa husaidia katika kilimo, ufugaji, uvuvi na uzalishaji wa umeme hivyo ni wajibu wa TANAPA kuvilinda kwa manufaa ya taifa.

TANAPA ni miongoni wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wanaoshiriki maonesho ya Kimataifa ya kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.