Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online,Geita
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, na kupewa maelezo ya kina kuhusu jinsi taasisi hiyo inavyonunua dhahabu kama njia mojawapo ya kuongeza akiba ya fedha za kigeni nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Afisa kutoka Idara ya Masoko ya Fedha ya BoT, Bi. Rehema Kassim, alisema kuwa ushiriki wa BoT katika maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu mchango wa benki hiyo katika ustawi wa uchumi wa taifa.
“Benki Kuu ni miongoni mwa wadau wakubwa wa sekta ya uchumi, na moja ya jukumu lake kuu ni kuhifadhi akiba ya fedha za kigeni. Moja ya nyenzo tunazotumia kufanikisha hilo ni ununuzi wa dhahabu, ili Serikali iweze kuwa na uwezo wa kifedha wa kufanikisha maendeleo ya nchi na wananchi kwa ujumla,” alisema Bi. Rehema.
Kwa mujibu wa Bi. Rehema, mwaka jana mwezi Oktoba, BoT ilianzisha mpango mkakati wa ununuzi wa dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wakubwa, kwa lengo la kuwapa fursa ya kuuza dhahabu moja kwa moja kwa Benki Kuu kwa bei ya ushindani ya kimataifa.
Mpango huo unaendana na kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, ambacho kinawataka wachimbaji wote wenye leseni kuuza asilimia 20 ya dhahabu wanayochimba kwa BoT. Kama motisha, wanapunguziwa malipo ya mrabaha kutoka asilimia 6 hadi 4, na ada kutoka asilimia 1 hadi 0.
Aidha, Bi. Rehema alieleza kuwa BoT imeweka mazingira rafiki zaidi ambapo wachimbaji hawalazimiki kuuza tu asilimia 20, bali wanaruhusiwa kuuza hadi asilimia 100 ya dhahabu yao kwa Benki Kuu, hatua inayochochea uwazi na ushindani wa bei sokoni.
Kwa sasa, uchimbaji wote wa dhahabu hupitia kampuni za uchenjuaji (refineries) zilizothibitishwa na BoT. Hadi sasa, BoT imeingia mikataba na kampuni tatu ambazo ni Geita Gold Refinery (GGR) ya Geita, Mwanza Precious Metals Refinery, na Isographica Refinery ya Dodoma. Uchimbaji unachagua refinery kulingana na ukaribu wa eneo lake na kampuni husika.
Hatua hii ya BoT inalenga si tu kuhakikisha ukusanyaji wa dhahabu kwa mujibu wa sheria, bali pia kuongeza akiba ya taifa ya rasilimali za thamani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza uchumi na kudhibiti mfumuko wa bei kupitia usimamizi madhubuti wa rasilimali za nchi.


Kwa upande wake Meneja Idara ya Mawasiliano wa BOT Vicky msina amemkabidhi Waziri Mkuu Majaliwa Zawadi sarafu ya Madini ya silver yenye thamani ya shilingi 50,000 kama kumbukumbu ambapo pia alimwomba awe mwalimu wa BOT wa kutoa elimu ya noti na sarafu na wanataka awe mwalimu wao wa kutoa elimu kwa wananchi namna ya kutunza noti na sarafu .

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina