January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu kuzindua UMITASHUMTA, UMISSETA leo

Dulla Makabila, Linah Sanga, Mzee Yussuf kutoa burudani

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo atafungua mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA) kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mashindano haya yanajumuisha Mikoa yote kutoka Tanzania Bara na Visiwani na yatafanyika kwenye viwanja vya Nangwanda Sijaona, Chuo cha Walimu Mtwara (TTC kawaida) Chuo cha Walimu Ufundi maarufu kama Mwasandube, na viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ufundi.

Katika mashindano hayo yatakayoanza leo hadi Julai 03 yanashirikisha washiriki 3,600 kutoka Mikoa yote Tanzania Bara kwa upande wa UMITASHUMTA na washiriki 3,800 kutoka Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar wanaoshiriki katika michezo ya UMISSETA.

Michezo itakayoshindaniwa kwa upande wa UMITASHUMTA ni mpira wa miguu kwa wasichana na wavulana, mpira wa miguu maalum kwa wavulana (wenye ulemavu wa kusikia) mpira wa pete, mpira wa goli kwa wasichana na wavulana wasioona na wenye uoni hafifu, mpira wa wavu kwa wasichana na wavulana, mpira wa mikono kwa wasichana na wavulana, mpira wa meza kwa wasichana na wavulana, riadha jumuishi, kwaya na ngoma.

Kwa upande wa UMISSETA michezo itakayochezwa ni yote ya UMITASHUMTA pamoja na mchezo wa mpira wa kikapu kwa wasichana na wavulana isipokuwa mchezo wa mpira wa goli, aidha kutakuwa na mashindano ya usafi katika mazingira wanayoishi.

Mashindano yatapambwa na wasanii wa kizazi kipya akiwemo Ibrah kutoka Konde Gang, Beka Flavour, Dulla Makabila, Linah Sanga na Peter Msechu na kwa upande wa taarabu atakuwepo Mzee Yussuf ambao wote watakuwepo ili kutoa hamasa na burudani.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, John Mapepele imeweka wazi kuwa, maandalizi yote kuelekea kwenye mashindano hayo yameshakamilika na kilichobaki ni uzinduzi rasmi utakaofanyika leo.

Juzi Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Kitaifa ya mashindano hayo, Yusufu Singo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisema, mashindano hayo yatasaidia kuvumbua vipaji na kupata wachezaji bora wa timu za Taifa kwa Michezo mbalimbali kwa miaka ya mbeleni.

Pia aliishukuru Serikali kwa kushirikisha Wizara tatu za Habari, TAMISEMI na Elimu kuratibu, kuandaa na kufanya mashindano haya ambapo alisema kwamba huo ni mkakati mzuri utakaosaidia kukuza sekta ya michezo kwa kasi.

Lakini pia wakati mashindano hayo yanatangazwa rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi alisema, viongozi wa mashirikisho na vyama vya michezo wanatakiwa kufuatilia mashindano hayo ili wajionee vipaji kwani mashindano hayo yatarushwa mubashara kupitia Televisheni mbalimbali nchini.

“Tutaendelea kuboresha michezo hii ili iwe kitovu cha kuandaa, kukuza na kuuza vipaji vya vijana wetu. Tunatana mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ya mwaka huu yabebe uhalisia wa tunachokimaanisha ili siku moja tuje tuwauze wanamichezo wetu chipukizi huko duniani,” amesema Dkt. Abbasi.

Kwa sasa zaidi ya wachezaji 26 katika Ligi Kuu (VPL) na Ligi ya Daraja la Kwanza (FDL) wametokana na mashindano hayo huku ikitoa takriban asilimia 95 ya wachezaji wa timu za soka za vijana.

Pia mashindano hayo ambayo ufunguzi wake utapambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali maarufu wa muziki wa kizazi kipya, kwa sasa yameboreshwa ili kuhama kutoka tukio la kawaida la michezo shuleni hadi kuwa tukio kubwa la kimichezo la kitaifa na kuwa kitovu cha mawakala wa vipaji kusaka nyota wa michezo mbalimbali.