March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10

Na Israel Mwaisaka,Rukwa

‎Waziri Mkuu, Dkt,Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajia kufanya ziara ya kikazi Mkoani Rukwa kuanzia Machi 8 hadi 10, 2026.

‎Akitoa taarifa ya ziara hiyo mbele ya waandishi wa habari leo Machi 7, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa  Charles Makongoro Nyerere, amesema ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inalenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kusikiliza wananchi kupitia mikutano ya hadhara.

‎Katika taarifa yake, RC  Makongoro ameeleza kuwa tarehe 8 Machi Waziri Mkuu atatembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga na Soko la Kimataifa la mazao Kanondo, na kisha kufanya mkutano wa hadhara katika Mji Mdogo wa Laela, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.

‎Tarehe 9 Machi Waziri Mkuu anatarajia kutembelea Wilaya ya Nkasi, kuweka jiwe la msingi la Shule ya Amali ya Mkoa iliyoko Namanyere na kufanya mkutano wa hadhara ambapo Pia atakagua Bandari ya Kasanga na kuzungumza na wananchi wa Kata ya Kasanga.

‎Ziara hiyo itahitimishwa tarehe 10 Machi kwa mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Ofisi ya Kata ya Majengo, Manispaa ya Sumbawanga.

‎Hivyo  Mkuu huyo wa Mkoa amewasihi wakazi, viongozi wa dini, viongozi wa kimila, viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa maendeleo kushiriki mikutano hiyo ili kupata ufafanuzi wa mambo mbalimbali yanayohusu shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali.

‎Ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi na kutathmini maendeleo ya miradi inayolenga kuboresha maisha ya wakazi wa Mkoa wa Rukwa.