September 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu atoa maagizo sita mkutano wa TRAMPA

Na Zena Mohamed,TimesMajira Online,Dodoma

WAZIRI Mkuu,Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa maagizo sita kwa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), akitaka wanachama wake kuhakikisha kumbukumbu na nyaraka zinalindwa na kutunzwa ipasavyo kwa manufaa ya Taifa.

Dkt. Nchemba pia ameitaka TRAMPA kuhakikisha historia ya Taifa inalindwa, pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi wanaofika katika ofisi za umma.

Aidha, ameagiza Taasisi za Umma kuanzisha vituo vya kisasa vya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, huku akisisitiza matumizi ya mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office) katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Ameitaka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kufuatilia mara kwa mara matumizi ya mfumo huo na kubaini ofisi ambazo hazitumii mfumo huo ili hatua zichukuliwe.

Vilevile, Dkt. Nchemba ameagiza Ofisi za Umma kuweka nguvu katika matumizi sahihi ya kumbukumbu na kutathmini utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Amesisitiza pia kuhakikisha watendaji wa TRAMPA wananufaika na ongezeko la mishahara la mwaka (Annual Salary Increment).

Maagizo hayo yametolewa leo Septemba 23, 2026, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, wakati akifungua wa Mkutano wa 14 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), jijini Dodoma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TRAMPA Taifa, Devotha Mrope amesema chama hicho kitaumia weledi kuhakikisha wanachama wake wanaimarisha usiri na ulinzi wa taarifa za Serikali na watumishi wa umma.

“Tunatarajia kuona Serikali ikihimiza matumizi ya teknolojia katika utunzaji wa kumbukumbu, hususani mfumo wa ‘e-Office’, pamoja na kuanzisha vituo vya kisasa vya utunzaji wa kumbukumbu na taarifa katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema Mrope.