March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu apongeza VETA kwa kuwawezesha vijana wenye ulemavu

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika maonyesho ya Wiki ya Vijana mkoani Mbeya, ambapo aliipongeza VETA kwa juhudi zake za kuwapatia ujuzi vijana wenye ulemavu.

Katika banda hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alijionea kazi mbalimbali zinazofanywa na vijana wakiwemo wenye ulemavu katika fani za kompyuta na ushonaji.

Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Mwalimu Francis Anthony ambaye pia ni Balozi wa Watu Wenye Mahitaji Maalum wa VETA, alisema kuwa yeye ni mhitimu wa fani ya kompyuta katika Chuo cha VETA Morogoro, ambako alipata pia mafunzo ya ualimu wa VETA.

“Mimi ni mhitimu wa VETA, na kwa sasa ni fundi wa kompyuta na mkufunzi mwenye ujuzi katika nyanja mbalimbali za ufundi,” alisema Francis.

Alisisitiza kuwa mafanikio yake ni ushahidi tosha kuwa vijana wenye mahitaji maalum wana uwezo mkubwa wa kujifunza na kuwafundisha wenzao.

Naye Riziki Ndumba, mwanafunzi wa VETA Songea anayesomea fani ya ushonaji, alieleza kuwa alijiunga na mafunzo hayo akiwa hana ujuzi wowote, lakini alipokelewa vyema na walimu pamoja na uongozi wa chuo.

Riziki alisema kuwa amemaliza kozi ya miaka miwili, na sasa anaamini anaweza kufanya kazi kama watu wengine, licha ya kuwa na ulemavu. Alitoa pongezi kwa VETA kwa kutambua uwezo wa watu wenye mahitaji maalum na kuwawezesha kwa vitendo

Akitoa maelezo katika banda hilo, Afisa Habari wa VETA, Eimer Sarao, alisema kuwa VETA imeendelea kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali ya vijana, wakiwemo waliomaliza vyuo vikuu ambao wameona umuhimu wa kurudi VETA kupata ujuzi wa kuwasaidia kujiajiri na kuwaajiri wenzao.

Vilevile, alisema kuwa wapo watu wenye ulemavu wanaopata mafunzo katika fani za kompyuta na ushonaji, na sasa wanafanya shughuli zao za kiuchumi kwa mafanikio.

“Tunao wahitimu wenye ulemavu akiwemo Francis Anthony, ambaye tulianza naye kuanzia ngazi ya kwanza (Level 1) hadi ya tatu (Level 3). Baada ya kuhitimu, hatukumwacha; tulimpeleka Chuo cha Mafunzo ya Ualimu wa Ufundi Stadi (MVTTC), ambako sasa amehitimu. Tunatembea naye kama ushuhuda kwamba kupitia mafunzo, hata walemavu wanaweza kupata ujuzi na kujiajiri,” alisema Sarao.