Na Mwandishi Maalum
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea hundi ya mfano ya sh. milioni 500 kutoka kampuni ya Export Trading Group (ETG) zikiwa ni msaada kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaotokana na maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19) nchini.
Waziri Mkuu alipokea msaada huo jana ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma, kutoka kwa Mkurugenzi mkazi wa ETG, Nilladri Chowdhury aliyefuatana na maofisa uhusiano wa kampuni hiyo, Frank Mtui na Fatma Salum Ally.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Waziri Mkuu aliwashukuru watendaji wa kampuni ya ETG kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona, ambapo hadi sasa kesi 49 zimeripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huo nchini.
“Kwa niaba ya Rais wetu John Magufuli tunawashukuru kwa msaada huu ambao utaisadia Serikali kupunguza makali ya kuwahudumia wananchi wetu. Tunahitaji kuungwa mkono na wadau wengine kama ninyi,” alisema.
Waziri Mkuu aliwataka wananchi wote wazidishe kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo hasa katika kipindi hiki. “Hatua tuliyofikia hivi sasa, maambukizi yameanza kuongezeka hasa kwa Dar es Salaam na Zanzibar. Tunajua kule kuna watu wengi na shughuli zote za kiuchumi zinaanzia pale, lakini hatuna budi kufuata masharti tuliyopewa ili kuzuia ugonjwa huu usisambae,” alisema.
“Serikali inatoa msisitizo kwa wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.”
“Muhimu zaidi sote tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu ili atupunguzie makali ya ugonjwa huu,” alisisitiza.
Mapema, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kampuni ya ETG, Mahesh Patel, Mkurugenzi Mkazi wa ETG, Nilladri Chowdhury alisema wameamua kuchangia fedha hizo ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika vita ya kupambana na ugonjwa huo.
“Mwenyekiti wetu amesafiri lakini kama kampuni, tumeamua kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu, na ametutuma tutoe mchango wa sh. milioni 500. Tuna imani na tunaendelea kumuomba Mungu ili atuvushe katika kipindi hiki,” alisema.
Alisema kampuni yao inashughulika na masuala ya kilimo zikiwemo kusambaza pembejeo na kuongeza thamani mazao kupitia kampuni yao ya Kapunga iliyoko Mbeya.
Pia inamiliki viwanda vitatu vya kubangua korosho vilivyoko Mtwara, Newala na Tunduru na viwanda vya kusindika mbegu za mafuta.Pia wanatoa soko kwa wakulima kwa kununua mazao kama vile korosho, mbaazi, kokoa, mahindi, choroko na ufuta.
Wakati huo huo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kuwaasa madereva wa vyombo vya usafiri kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Maji na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anyitike Mwakitalima wakati wa uhamasishaji wananchi kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona katika mikoa ya Mbeya na Songwe.
Alisema kila dereva na kondakta wake ni lazima wahakikishe gari linakuwa na vitakasa mikono (Sanitizer) kwa ajili ya matumizi yao na abiria.
Aidha, vituo vyote vya mabasi vimetakiwa kuwa na sehemu za kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kwani hiyo ni hatua muhimu sana katika kujikinga na virusi vya Corona.
Aliyasema hayo alipotembelea Stendi Kuu ya mabasi katika Jiji la Mbeya iliyopo eneo la Nane Nane.
“Kondakta hakikisha kila anayepanda gari lako amenawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka au ametakasa mikono yake kwa Sanitizer ndio aruhusiwe kuingia kwenye gari, huu ugonjwa jamani ni hatari na umeua watu wengi,” alisema.
Aidha, aliwaagiza madereva na makondakta wao kuhakikisha kila siku jioni wanapokuwa wamemaliza kazi zao wahakikishe wanasafisha magari yao kwa dawa maalum aina ya Jiki ili kuua virusi vinavyoweza kuwepo na kupelekea maambukizi ya Corona.
“Madereva na makondakta wote kila siku jioni, hakikisha mnasafisha magari yenu kwa dawa maalum, wote mnaifahamu Jiki hapa, dawa hii inatumika Kutakasa magari, bajaji au pikipiki. Changanya kipimo kimoja cha Jiki na vipimo sita vya maji ili kupata mchanganyiko unaotakiwa kisha osha chombo chako cha kusafirisha abiria, utajikinga wewe na abiria wako ” alisema.
Naye Ofisa kutoka Makao Makuu Jeshi la Polisi Kamisheni ya Ushirikishaji Jamii Stafu Sajenti Valentino Ngowi, aliwataka madereva bodaboda kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi endapo watakutana na mtu aliyeingia nchini kwa njia za panya, ikiwa ni moja ya jitihada za kupambana na ugonjwa wa Corona, huku akiwataka wasiingie katika vishawishi vya kutaka pesa ya haraka ambayo inaweza kuwagharimu wao na taifa kwa jumla.
“Sasa hivi kuna abiria wengi ambao wanaingia mkoani Mbeya kupita njia za panya, na njia rahisi wanayotumia ni watu wa Bodaboda, hivyo tunawata msiingie kwenye vishawishi vya kutafuta hela ya haraka kwa kuwapitisha watu hao, jambo ambalo ni kinyume na Sheria,” alisema
Mbali na hayo, Stafu Sajenti Valentino Ngowi aliwataka madereva wote wa vyombo vya moto kuhakikisha wanafuata sheria bila shurti, ikiwemo kuhakikisha abiria hawasimami kwenye magari (level seat), huku kwa upande wa Bajaj wapande abiria watatu tu.
Kampeni hii ya mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana ya Shirika lisilo la kiserikali la Project Clear.
Katika kuchagiza ufikishaji wa elimu ya tahadhari dhidi ya Corona, Wizara inashirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery, ambaye aliwakumbusha wakazi wa Jiji la Mbeya hususani maeneo ya Uyole, Sae, Ilomba, Mwanjelwa, Stendi Kuu, Meta, Nzovwe na Mbalizi kuzingatia unawaji wa mikono kwa maji na sabuni na vile vile kuepuka kushikana mikono na misongamano isiyokuwa na lazima.
Ziara hii ya utoaji wa elimu ya tahadhari dhidi ya Corona inaendelea katika Mkoa wa Songwe ambao unapakana na nchi ya Zambia.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best