December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu aongoza mazishi ya Mwenyekiti CCM Tabora

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

ALIYEKUWA Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Tabora Hassan Mohamed Wakasuvi amepumzishwa katika nyumba yake ya milele leo katika Kijiji cha Mabama, Kata ya Mabama, Wilayani Uyui Mkoani Tabora.

Akiwasilisha salamu za serikali mbele ya maelfu ya waombolezaji wakiwemo wanaCCM, Viongozi wa Chama na Serikali, Wakuu wa Taasisi na Mashirika mbalimbali na wakazi wa Mkoa huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Samia amehuzunishwa sana na kifo cha Mzee wakasuvi.

‘Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amewapa pole sana wafiwa wote, wanaCCM na wakazi wa Mkoa wa Tabora, alitamani sana kuwepo hapa lakini yupo nchini Namibia kwenye msiba mwingine wa Rais wa nchi hiyo’, ameeleza.

Amebainisha kuwa marehemu ametoa mchango mkubwa sana katika sekta ya kilimo hapa nchini hasa kutokana na umahiri na uzoefu wake mkubwa katika masuala ya ushirika, hili lilipelekea kushika nyadhifa mbalimbali katika Bodi za Vyama vya Ushirika na Tume ya Ushirika ndani na nje ya nchi.

Amesisitiza kuwa serikali haitamsahau kamwe kwa utumishi wake uliotukuka ndani ya chama ikiwemo ushauri na mchango mkubwa aliotoa kwa serikali ambao ulichochea kwa kiasi kikubwa juhudi za serikali kuwaletea maendele wananchi.

Amewataka wanafamilia kuwa wamoja na kuishi kwa amani huku akiwahakikishia kuwa serikali ipo pamoja nao na itaendelea kufanya kila linalowezekana pale itakapotakiwa kufanya hivyo.

Akitoa salaamu za Chama, Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt Emanuel Nchimbi amesema kuwa Chama kimepoteza Kiongozi makini, shupavu na mpenda maendeleo.

Ameongeza kuwa weledi, hekima na uchapakazi wake vilikuwa chachu kubwa ya maendeleo ndani ya chama na serikali, ndiyo maana Chama kilimwamini na kumpa majukumu katika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Ujumbe wa Kamati Kuu.

Amebainisha kuwa marehemu Wakasuvi (70) enzi za uhai wake mbali na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa CCM Mkoa pia alitumikia nafasi mbalimbali ndani ya Chama na Jumuiya ya Vijana ikiwemo Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Chama na Mlezi wa CCM Mkoa wa Arusha.

Dkt Nchimbi amefafanua kuwa kutokana na uchapakazi wake mzuri tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora mwaka 2007 alifanya kazi kubwa sana ya kuimarisha chama na kuunganisha wanaCCM wote.

Amewataka wanaCCM wote Mkoani hapa na jamii kwa ujumla kumuenzi kwa kudumisha amani, utulivu na mshikamano ili chama kiendelee kuwa na nguvu zaidi kama ilivyokuwa enzi za Mzee Wakasuvi.