Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Profesa, Kitila Mkumbo amezindua Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (BRELA ) yenye wajumbe watano ambapo ameitaka kuhakikisha inasimamia menejimenti ya shirika hilo ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira mazuri ya Biashara.
Bodi hiyo yenye wajumbe watano inayoongozwa na Mwenyekiti Profesa Neema Mori ambaye ni Profesa wa Masuala ya Biashara kutoka shule kuu ya chuo Kikuu cha Dar es salaam, Judith Kadege, Allen Kasamala ambaye ni mwanasheria , Elias Kalisti, pamoja na Dkt. Fred Msemwa.
Akizungumza na waandishi habari mkoani Dar es salaam wakati wa utambulisho wa wajumbe hao Profesa, Mkumbo amesema majukumu makubwa ya bodi hiyo ni kumshauri na kusimamia masuala mazima ya Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (BRELA).
“Kwa mujibu wa sheria ya wakala ya Serikali ya mwaka 1997 pamoja na marekebisho yake yaliyofanyika mwaka 2009 inampa waziri wa Viwanda na Biashara mamlaka ya kuteua bodi ya ushauri ambayo itakuwa inamshauri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Taasisi husika ambayo ni BRELA” amesema Profesa Mkumbo.
Amesema ili kuondoa vikwazo vya kibiashara bodi hiyo inajukumu la kuhakikisha Usajili wa biashara unapita bila ya kikwazo chochote .
“Tanzania tunabiashara nyingi zisizo rasmi takribani Biashara ndogo ndogo na za kati Millioni 3 na laki 7 ambapo kati ya hizo ni asilimia 4 pekee ndio zimesajiliwa, kurasimisha biashara kunaanza na biashara kusajiliwa na watu kuunda Makampuni watu wengi Tanzania wanafanya biashara kama mtu binafsi awajaunda Makampuni hivyo wajumbe wa bodi mnalo jukumu la kuhakikisha mnalisimamia suala hili “amesema Profesa Mkumbo.
Amesema ili kuzalisha ajira ni lazima kuhakikisha biashara za Tanzania zinasajiliwa na kuwa rasmi kufanya hivyo kutasaidia watu kulipa kodi na kujiajiri.
Majukumu ya msingi ya bodi hii ni kunishauri kwenye mambo ya menejimenti ya shirika letu kwasababu kwa sasa BRELA ni Taasisi muhimu sana katika mpango mkubwa wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuboresha mazingira ya biashara hapa Tanzania”amesema Profesa Mkumbo.
Pia amesema kwa sasa biashara zimeingia katika mtandao na kutokana na kuwepo kwa Ugonjwa wa virusi vya corona UVIKO 19 BRELA ipo katika mchakato wa kujiendesha kimtandao zaidi.
Aidha amesema bado kuna chagamoto ya takwimu katika taasisi hiyo ambapo ameagiza Bodi hiyo kuhakikisha baada ya miezi mitatu kuwe na Takwimu zote za msingi na ziwe na mfumo rahisi wa upatikanaji wa Takwimu.
Hata hivyo Profesa Mkumbo ameiagiza bodi hiyo ikae na kufanya uchambuzi kuhusu sheria kadhaa ikiwemo sheria mama ya makampuni ambayo wadau wamekua wakiilalamikia ikionekana baadhi ya vipengele kupitwa na wakati na kuona ni kiwango gani wanahitaji kufanya marekebisho katika sheria hiyo na kama inahitaji kuandikwa upya wamshauri aisogeze katika ngazi ya serikali na hatimaye ipelekwe bungeni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi hiyo Profesa Neema Mori amemshukuru Waziri Mkumbo kwa kuwaamini wote na kuwapatia nafasi katika bodi hiyo mpya na kumuhaidi kutoa Ushirikiano kwake na Menejimenti nzima ya BRELA.
More Stories
Kamati ya Mfuko wa Jimbo Musoma Vijijini yagawa vifaa vya ujenzi
Hatma mrithi wa Kinana kupatikana
Mrithi wa Kinana CCM kujulikana katika Mkutano Mkuu wa Jan 18/19