November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkenda asisitiza umuhimu wa VETA kushirikiana na waajiri

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesisitiza umuhimu wa taasisi za mafunzo kama VETA (Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi) kushirikiana moja kwa moja na waajiri katika uundaji wa mtaala na uhamasishaji wa ujuzi ili kuboresha umuhimu wa kozi zinazotolewa

Amesema ushirikiano huo ni muhimu ili kuunda mtaala unaoendana na mahitaji ya soko la ajira na kusaidia wanafunzi kupata ujuzi unaohitajika katika ajira halisi lengo ikiwa ni kuhakikisha kuwa kozi zinazotolewa zinasaidia wahitimu kupata ajira na kujitegemea kiuchumi.

Hayo ameyasema katika mkutano wa TVET uliofanyika jana Jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kwa kufanya hivyo, wahitimu wa mafunzo hayo wataweza kupata ajira kwa urahisi zaidi na kuchangia katika maendeleo ya taifa.

“Ajira ni bomu mubwa kwa Afrika nzima, kumekuwa na kundi kubwa na wastani wa kuishi umeongezeka, watoto watakua watafika umri wa miaka 20 wataanza kutafuta kazi”

“Rais Samia alisisitiza elimu yetu iandae watu waweze kuajirika , pia Rais samia amepambana kufanya uwekezaji hasa kwa kujenga viwanda ili vijana waweze kuajiriwa. Changamoto iliyopo ni kutokujenga daraja madhubuti la kuunganisha uzalishaji na mafunzo” alisema

Aidha Prof. Mkenda amesistiza kuwepo kwa mabadiliko ndani ya Mamlaka ya Elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) huku akisisitiza ukuhimu wa kuimarisha ubora wa mafunzo yanayotolewa VETA ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuendeleza ustawi wa vijana wa kitanzania.

“Kupitia mabadiliko haya, VETA inapaswa kutoa mafunzo bora na yenye kuendana na teknolojia za kisasa ili vijana waweze kuwa na ujuzi unaotakiwa kimataifa”

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Nchini (ATE) Suzan Ndomba-Doran amesema chama hicho kina mpango wa kuanzisha mabaraza ya ujuzi ili kushirikiana na wadau wengine kukuza kiwango cha ujuzi kwa vijana pamoja na uwezo wa vyuo vya ufundi na vyuo vikuu ili kuzalisha vijana wengi zaidi wenye ujuzi.

Amesema, asilimia 79 ya nguvu kazi nchini ina ujuzi wa chini au haina ujuzi wa kutosha katika kuendeleza maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kwani asiliia 34.7% ya watanzania ni vijana kati ya miaka 15-35. Lakini wengi wao wanakutana na changamoto za kukosa ujuzi ambazo upelekea kushindwa kujiajiri au kuajiriwa.

“katika kukabiliana na hilo, ATE kwa kushirikiana na Shirikisho la Viwanda vya Denmark na cha Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Wakala wa Maendeleo ya Vyama vya Wafanyakazi Denmark (DTDA) na washirika (Tanzania Union of Industrial and Commercial workers -TUICO & Researchers Academicians and Allied Workers Union – RAAWU), tunatekeleza mradi huu wa TVET unaolenga kukuza ujuzi ili kutengeneza vijana wanaoweza kuajiriwa wenye ujuzi wa ufundi stadi na ajira zenye staha nchini.

Amesema mpaka sasa mradi huo ulioanza mwaka 2021 umefanikiwa kupata mafanikio kadhaa pamoja na mambo ya kujifunza kwa ajili ya kuboresha ambapo wamepitia na kurejea mitaala kulingana na mahitaji ya soko kwa Fitter mechanics, umeme wa Majumbani na Viwandani, Uzalishaji wa Chakula, Majokofu na viyoyozi.

“pia tumetoa mafunzo kwa jumla ya wanafunzi 1098 ambapo asilimia 43 ni wanawake na asilimia 57 ni wanaume kwa aina mbili za uanagenzi kwa kushirikiana na washirika huku pia mafunzo mengine yakitolewa kwa wakufunzi katika eneo la kazi kwa muda wa wiki mbili ili waweze kujifunza teknolojia mpya pamoja na kulinganisha wanachokifundisha chuoni na uhalisia wa soko” amesema Doran.

Naye, Katibu Mkuu wa Raawu, Joseph Sayo amesema pamoja na kwamba mradi umepata mafanikio ya kuongeza ujuzi kwa vijana katika sekta mbali mbali ikiwemo baadhi yao kupata ajira lakini kunahitajika kuendelea kuwekeza katika mafunzo ya ufundi stadi ili kihakikisha vijana wetu wanauwezo wa kushindana katika soko la ajira.

“Ujuzi unaotolewa katika vyuo vyetu umekuwa hauendani na Teknolojia iliyopo viwandani kwa sasa kitu kinachopeleka vijana wengi kushindwa kuajiriwa katika viwanda vyetu kwa kuwa ujuzi walionao wameupata kupitia mashine ambazo zimepitwa na wakati na hivyo wakifika viwandani wanaenda kujifunza upya.

“Tunaiomba serikali kupitia Wizara Elimu isaidie katika kuhakikisha vyuo vya ufundi vinapata nyenzo sahihi za kufundishia na kujifunzia ili vijana waweze kuendana na kasi ya soko la ajira duniani.

Aidha ameishuruku serikali ya Denrmark kwa kufadhili mradi huo uliopata mafanikio makubwa hivyo wanatumaini lwa ushirikiano huo, vyul vyetu vitaimarika zaidi na kuhakikisha vijana wanajifunza kwa nadharia na vitendo ili waweze kuhitimu wakiwa na na ujuzi unaohitajika katika kuajiriwa ama kujiajiri.

Katika kongamano hilo, waajiri ambao walichukua wanafunzi wengi zaidi kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na Taasisi tano walitunukiwa vyeti.