November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mhagama akagua usimikaji mifumi ya usalama mgodi Shanta

Na Bakari Lulela, TimesMajira,Online,Ikungi

WAZIRI wa Nch Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu) Jenista Mhagama amefanya ziara katika mgodi wa dhahabu wa Shanta uliopo wilaya ya Ikungi mkoani Singida kwa lengo la kukagua usimikaji wa mifumo ya usalama na afya katika hatua za awali za maandalizi ya uchimbaji madini katika mgodi huo.

Waziri amesema ni muhimu kwa sehemu mbalimbali za kazi zinazoanzishwa hapa nchini ikiwemo migodi kuwahusisha wataalamu wa usalama na afya katika hatua za awali za ujenzi wa miundombinu.

Amesema hatua hiyo itawawezesha kupata ushauri utakaowawezesha kujenga miundombinu inayozingatia viwango vya usalama na afya mahali pa kazi, hivyo kuepuka kuweka miundombinu ambayo ipo kinyume na sheria na kanuni za usalama na afya mahali pa kazi.

“Kwetu sisi na wenzangu wa OSHA tutakachojitahidi ni kuendelea kuwapa elimu ya kutosha kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ili mbobee kwenye eneo hilo kusudi muondoshe migogoro katika eneo lenu la kazi na ndio maana ninaomba muwaruhusu hapa wawe na tawi la wafanyakazi.

Lakini tutawasaidia pia kukagua na kuangalia mifumo yenu ya usalama na afya kama itaweza kulinda afya za wafanyakazi hususan pale mtakapo anza rasmi uzalishaji, kwani tunatambua kwamba shughuli hizi za uchimbaji madini huambatana na vihatarishi vingi vya usalama na afya ambavyo vinahitaji mifumo madhubuti ya kukabiliana navyo,” amesema Jenista Mhagama.

Akiwa ameambatana na Waziri Mhagama katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Usalama na Afya wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi OSHA, Mhandisi Alexander Ngeta, ametoa wito kwa kampuni kubwa ambazo zinafanya kazi na kampuni saidizi(sub-contractors) kuhakikisha kwamba makampuni hayo yanazingatia sheria na kanuni za usalama na afya mahali pa kazi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, akikagua maeneo ya mgodi mpya wa dhahabu wa Shanta uliopo Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida alipofanya ziara ya kukagu usimikaji wa mifumo ya Usalama na Afya katika mgodi huo kabla ya kuanza rasmi shughuli za uchimbaji zinazotarajiwa kuanza mwakani. Alioambatana nao ni Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Mhandisi Jiten Divecha (kushoto), Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtatulu (kulia) pamoja na viongozi wa Wilaya ya Ikungi na baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo.

Awali akiwasilisha taarifa yake kuhusu hali ya usalama na afya katika mgodi huo mbele ya Waziri, Mkurugenzi wa usalama wa OSHA, Mhandisi Ngata ameeleza kwamba kampuni hiyo imekuwa ikijitahidi kutekeleza matakwa yote ya sheria ya Afya na Usalama Mahali pa kazi kama ambavyo wamekuwa wakielekezwa na wataalamu kutoka OSHA.

Aidha amebainisha kwamba changamoto iliyopo ni kwa makampuni saidizi (sub -contractors) yanayofanya kazi na Shanta ambayo bado hayazingatii utekelezaji wa sheria tajwa.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida,Tabora na Kigoma, Venance Buliga amesema wamekuwa wakishirikiana ipasavyo na uongozi wa mgodi huo katika hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya uchimbaji madini.

Amesema wamekuwa wakifanya ukaguzi na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kujenga miundombinu inayozingatia afya na usalama wa wafanyakazi.

Aidha, Menejimenti ya mgodi huo pamoja na wafanyakazi wameeleza kuwa usalama na afya kwa wafanyakazi ni miongoni mwa vipaumbele vya Kampuni hiyo.

“Tunafanyakazi kwa kuzingatia misingi mitatu ambayo ni biashara,mahusiano na jamii inayotuzunguka pamoja na afya na usalama wa watu wetu kama tulivyoeleza katika taarifa yetu kwa Waziri na yeye pamoja na wataalamu wa OSHA wamethibitisha hilo walipotembelea sehemu mbalimbali katika mgodi,” amesema Mhandisi Jiten Divecha, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Shanta wa Ikungi Mkoani Singida.

“Kwa masuala ya usalama na afya hapa Shanta tuko vizuri sana, kila sehemu ambayo watu wafanyakazi masuala ya matumizi sahihi ya vifaa kinga yanazingatiwa ipasavyo na pia wakaguzi wa OSHA huwa wanatutembelea kuangalia namna tunavyofanya kazi na kutushauri kuboresha endapo tunakuwa kinyume na taratibu za usalama na afya mahali pa kazi,” amesema Ferdinand Cyprian mfanyakazi wa mgodi wa Shanta Ikungi katika kitengo cha upakaji rangi majengo.

OSHA ambayo ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) inadhamana ya kusimamia utekelezaji wa sheria ya afya na usalama mahali pa kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake ambayo pamoja na mambo mengine inawataka wamiliki wa sehemu za kazi nchini kusajili maeneo yao na OSHA kufanyiwa ukaguzi wa usalama na afya kuchunguza afya za wafanyakazi pamoja na kuwapa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi.